Rodgers Oloo aliwaokoa mwewe mitaani na sasa hawamuachi kila aendapo/ Picha: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Ukistaaju ya Musa utaona ya Firauni.

Katika mitaa ya jiji la Nairobi huko nchini Kenya, kijana mmoja ameibuka na kujipatia jina la ‘Bird man’ yani mtu wa ndege.

Hii ni baada ya kijana huyo, kuwa kivutio cha wengi baada ya kuonekana mitaani akiambatana na ndege mwewe.

Wengi wanashikwa na butwaa wanapomuona Rogers Oloo akivinjari mitaa ya jiji la Nairobi na mwere ambao hawamuachi kila aendapo.

Akisimulia mwanzo wake, Rodgers anasema katika pita pita yake mitaani Januari mwaka huu, alimuona mwewe mtini akiwa amedhoofika.

Akaamua kumpa kipande cha kuku alichokuwa amepewa na msamaria mwema.

Baadaye akaona watu wanataka kumua nae akaamua kumuoakoa. Na hapo ndipo urafiki wao wa ajabu ulipoanza.

Alimuita mwewe wake wa kwanza “Johnson the hawk.”

Baada ya muda marafiki wakaongezeka, akapata wengine wawili ambao pia aliwatunza kwa kuwapa chakula na kuishi nao.

Hata hivyo mmoja alikufa. Umaarufu wa Rodgers uliongezeka hasa alipoonekana na mwewe wake katika maandamano ya Gen Z mnamo mwezi Juni na Julai.

Watu wengi mpaka sasa hawaelewi jinsi ndege hawa maarufu kama “wezi wa kuku” wanavyoweza kuishi na binadamu.

Wengine wanamuhusisha na imani za ushirikina lakini mwenyewe anakana tuhuma hizo.

Ingawa mwewe anajulikana kwa kula nyama sana, hawa wa Rodgers wamefunzwa kupambana na hali ya mitaani.

Anasema amewafunza kula matunda kama parachichi na machungwa na hata mahindi.

Lakini urafiki wa Rogers na mwewe umeleta fursa kwake kwani watu wengi wanamtafuta kupiga picha naye na wengien kumchangia/ Picha: Reuters 

Anaasema wamebadilisha maisha yake kwani watu hawamwangalii tena kwa shauku kama kijana wa mitaani.

Lakini urafiki wa Rogers na mwewe umeleta fursa.

Watu wameanza kumdhamini na kumtafuta kwa shauku ya kutaka kujua anavyoweza kuishi na ndege.

Huku wengine wakitaka kupiga nae picha, na wengine wakimchangia hapa na pale. Rodgers anasema hawezi kukubali mwewe hawa wachukuliwe kwani wao ndio rafiki zake wa kweli.

TRT Afrika