Na Coletta Wanjohi
Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali, IGAD imeazimia kuwatuma marais Salva Kiir wa Sudan Kusini, William Ruto wa Kenya na Ismaïl Omar Guelleh wa Djibouti kuwa mpatanishi katika mzozo unaoendelea nchini Sudan.
IGAD inajumuisha nchi ya Kenya, Somalia, Sudan, Djibouti, Sudan Kusini, Uganda na Ethiopia.
Mzozo mkali unaendelea kati ya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF) tangu tarehe 15 Aprili.
“Rais Salva Kiir Mayardit yuko katika mawasiliano ya karibu na viongozi wa Sudan kwa matumaini kwamba hali ya sasa ya kudorora itaafikiwa,” ilisema taarifa iliyotolewa na serikali ya Sudan Kusini,”
Sudan Kusini ilisimamia makubaliano ya Juba, mkataba wa amani uliotiwa saini tarehe 3 Oktoba 2020 kati ya serikali ya Sudan na muungano wa Sudan Revolutionary Front na makundi mengine ya kisiasa, ulifanikiwa kwa kiasi kusimamisha uhasama kati ya pande hizo mbili.
"Tunaziomba pande zote kutatua tofauti zozote kwa njia za amani kwa ajili ya usalama wa watu wa Sudan na utulivu nchini na kandani," rais wa Kenya William Ruto amesema kwenye mtandawo wa twitter.
"Hatuwezi kuendelea kuandika makosa ya siasa zisizo na kanuni mwaka baada ya mwaka," rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema katika mkutano wa dharura wa IGAD, Jumapili, " Sudan kusitisha uhasama bila masharti na mara moja ni muhimu ili kukomesha janga na kejeli ya Afrika.”
Mamlaka ya IGAD inasema mzozo huo "unadhoofisha maendeleo ya amani yaliyopatikana katika kipindi cha miezi minne iliyopita, nchini Sudan.”Viongozi hao pia waliyataka makundi hayo mawili kutoa njia salama kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu huko Khartoum na miji mingine iliyoathiriwa.
Kwa nini utulivu nchini Sudan ni muhimu kwa kanda?
Majirani wa Sudan wanapambana na mizozo yao wenyewe hivyo vita nyingine inaweza kuwa ngumu kwao. Sudan inapakana na Ethiopia.Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linasema kuna zaidi ya wakimbizi 56,000 wa Ethiopia wanaohifadhiwa nchini Sudan.
Hawa ni watu waliokimbilia usalama katika kilele cha mzozo kati ya serikali na chama cha Tigray People's Liberation Front kilichoanza Novemba 2020. Makubaliano ya amani yalitiwa saini kati ya wawili hao mnamo 2022.
Ethiopia pia ina mzozo wa muda mrefu wa mpaka na Sudan katika eneo linaoitwa Al-Fashaga. Ni sehemu ya mpaka wa kaskazini kati ya Ethiopia, Sudan na Eritrea na imekuwa kielelezo katika muongo mmoja uliopita kati ya Sudan na Ethiopia.
Sudan pia inazozana na Ethiopia kuhusu bwawa megawati 6000 ambalo Ethiopia inajenga kwenye Mto Nile.
Sudan na Misri, mataifa mawili yaliyo chini ya mto Nile, yanataka makubaliano ya kisheria juu ya kujaza na uendeshaji wa GERD, matakwa yanayo pingwa na Ethiopia.
Sudan Kusini ambayo ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011 ina changamoto na mzozo wake wa ndani.
Mnamo mwaka wa 2018, ghasia kati ya wanajeshi wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar ziliweka msingi wa vita, Umoja wa Mataifa unauita mzozo wa kibinadamu, zaidi ya miaka kumi baadaye.
Umoja wa Mataifa unasema mzozo wa kibinadamu nchini humo sasa unalazimisha takriban watu milioni 9.4, kuwa katika ukingo wa kutegemea misaada ya kibinadamu.
Makubaliano ya amani kati ya makundi yanayopigana katika serikali ya mpito ya Sudan Kusini mwaka 2019 yaliainisha umuhimu wa kupata katiba mpya, kuunganisha makundi mbalimbali ya kijeshi katika kitengo kimoja, na njia ya kupanga uchaguzi mpya.
Chad ilifunga mipaka yake na Sudan tarehe 15 Aprili 2023, wakati mapigano yalipoanza kati ya jeshi la Sudan na vikosi vya msaada wa haraka vya kijeshi.
Chad iko chini ya utawala wa kijeshi tangu Aprili 2021, wakati rais wa Chad Idriss Deby Itno aliuawa kwenye vita na waasi. Mtoto wa raisi huyo Mahamat Idriss Deby alichukua madaraka. Baraza la kijeshi alilounda liliahidi kipindi cha mpito cha miezi 18 hadi uchaguzi lakini mnamo 2022 waliongeza uchaguzi hadi Oktoba 2024.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika kikao chake cha dharura siku ya Jumapili lilisisitiza kwamba halitakubali "uingiliaji wowote wa nje ambao unaweza kuharibu zaidi hali ya Sudan"
Shirika la Afya Ulimwenguni linasema tangu Aprili 13, zaidi ya watu 83 wameuawa na zaidi ya watu 1126 wamejeruhiwa kote Khartoum, Kordofan Kusini, Darfur Kaskazini, Jimbo la Kaskazini na mikoa mingine.