Iran imetoa wito kwa mataifa ya G7 kujitenga na "sera za uharibifu za siku za nyuma," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanaani alisema, akimaanisha taarifa ya G7 kulaani kuongezeka kwa mpango wa nyuklia wa Iran hivi karibuni.
Siku ya Ijumaa, G7 iliionya Iran dhidi ya kuendeleza mpango wake wa kurutubisha nyuklia na ikasema itakuwa tayari kutekeleza hatua mpya ikiwa Tehran itahamisha makombora ya masafa marefu hadi Urusi.
"Jaribio lolote la kuhusisha vita vya Ukraine na ushirikiano wa pande mbili kati ya Iran na Urusi ni kitendo chenye malengo ya kisiasa yenye upendeleo," Kanaani alisema siku ya Jumapili, na kuongeza kuwa baadhi ya nchi "zinaegemea kwenye madai ya uwongo ya kuendeleza vikwazo" dhidi ya Iran.
Wiki iliyopita, Baraza la Magavana la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia lenye nchi 35 lilipitisha azimio la kuitaka Iran kuongeza ushirikiano na shirika hilo na kubatilisha uzuiaji wake wa hivi karibuni wa wakaguzi.
Iran ilijibu kwa kuweka haraka mitambo ya ziada ya kurutubisha uranium kwenye tovuti yake ya Fordow na kuanza kuweka vingine, kulingana na ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
Kanaani aliongeza kuwa Tehran itaendeleza "maingiliano yake ya kujenga na ushirikiano wa kiufundi" na IAEA, lakini ilisema azimio lake "lina upendeleo wa kisiasa."
Iran sasa inarutubisha uranium hadi kufikia asilimia 60 ya usafi, karibu na asilimia 90 ya daraja la silaha, na ina nyenzo za kutosha zilizorutubishwa kwa kiwango hicho, ikiwa zimerutubishwa zaidi, kwa silaha tatu za nyuklia, kulingana na kipimo cha IAEA.