Tanzania imeanza juhudi za kuongeza ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini kupitia Jukwaa la Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, lililofanyika jijini Mwanza, likiwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi.
Jukwaa hilo limewaleta pamoja wataalamu, wawekezaji na wadau wa sekta ya madini kutoka Tanzania, Ghana na Afrika Kusini kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuhakikisha rasilimali za madini zinakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi.
Kwa mtazamo wa kimataifa, mjadala unaojengwa katika jukwaa hilo unaangazia changamoto inayozikabili nchi nyingi za Afrika — namna ya kuondokana na utegemezi wa kuuza madini ghafi na badala yake kuongeza thamani kupitia uchakataji, teknolojia, viwanda na ajira kwa wananchi.
Wadau wanasema uelewa mpana wa sekta ya madini ni hatua muhimu kwa Watanzania kushiriki katika ushindani wa kimataifa, kwani fursa zilizopo ndani ya sekta hiyo zinahitaji maarifa, mitandao na uwezo wa kuwekeza.
Akizungumza na TRT Afrika, Dkt. Zainab Katima, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema majukwaa kama haya yanasaidia kuwawezesha wadau wa ndani kuelewa mwenendo wa sekta ya madini na kujiandaa kushiriki katika fursa za kimataifa.
“Hatuwezi kuvuka kwenda mataifa kama hatuna uelewa na vitu vinavyotokea nchini. Majukwaa kama haya ni muhimu kwa wadau nchini kuelewa sekta hii ikoje na kuweza kuvuka kwenda mbele.”
Kwa upande wake, Godfrey James, Mwanasheria na Mdau Mshiriki wa Jukwaa, amesema kuna umuhimu wa kuongeza majukwaa kama hayo ili kuwafanya Watanzania wengi zaidi kufahamu fursa zinazopatikana katika sekta ya madini.
Amesema dhana kwamba sekta ya madini ni kwa wawekezaji wakubwa pekee inahitaji kubadilika, akieleza kuwa sera za uwekezaji pamoja na sheria ya Local Content zimefungua nafasi kwa Watanzania kushiriki zaidi.
“Tungependa majukwaa kama haya yafanyike mara nyingi zaidi ili kuichochea sekta ya madini na kumfanya Mtanzania wa kawaida ajue nini kinaendelea na aweze kuwekeza kwenye madini.”
Waziri wa Madini Tanzania na mgeni rasmi katika jukwaa hilo, Anthony Mavunde, amesema Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utoaji wa huduma za migodini katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku ikiweka mkazo katika kuongeza nafasi ya Watanzania ndani ya mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
“Lengo letu kama Wizara ni kuifanya Tanzania iwe kitovu cha utoaji wa huduma migodini Kusini mwa Jangwa la Sahara. Tusiishie Tanzania tu, tuvuke na mipaka ya Tanzania.”
Sekta ya madini imeendelea kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania, ikichangia mapato ya Serikali, ajira na uwekezaji. Hata hivyo, mjadala mkubwa unabaki katika kuhakikisha wananchi wanapata nafasi kubwa zaidi katika huduma za migodini, uchakataji wa madini na biashara ya rasilimali hizo.
Kupitia jukwaa hili, Tanzania inalenga kujijenga kama mshiriki muhimu katika ramani ya madini barani Afrika, kwa kuhakikisha rasilimali zake zinatumika zaidi kukuza viwanda, teknolojia na maendeleo endelevu.














