Mtoto wa Mugabe akiri kumtishia mtu kwa bunduki nchini Afrika Kusini

Bellarmine Chatunga Mugabe, 29, alikamatwa na polisi kwa madai ya jaribio la kuua kufuatia tukio la kufyatua risasi jijini Johannesburg.

By
Bellarmine Chatunga Mugabe, mtoto wa aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe, akiwa mahakamani jijini Johannesburg, Afrika Kusini. / Reuters

Mtoto wa mwisho wa kiongozi wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe amekiri kosa siku ya Ijumaa la kumtishia mtu kwa bunduki na kuwepo nchini Afrika Kusini kinyume cha sheria lakini akakanusha kuwa alifyatua risasi na kumjeruhi mtengeneza bustani wake baada ya kugombana.

Bellarmine Chatunga Mugabe, 29, alikamatwa na polisi yeye pamoja na binamu yake ambaye ni mshtakiwa mwenzake, Tobias Mugabe Matonhodze, kwa madai ya jaribio la kuua kufuatia tukio hilo katika mtaa wa kifahari wa Hyde Park, jijini Johannesburg.

Mugabe alikiri kuwa Afrika Kusini kinyume cha sheria na kumtishia mtu bunduki katika tukio lingine, ilhali Matonhodze alikiri jaribio la mauaji.

Matonhodze, 32, pia alikiri kukiuka sheria za uhamiaji pamoja na za kumiliki silaha.

‘Majadiliano hayakufanikiwa’

"Awali tulikuwa tumezungumza na serikali kwa lengo la makubaliano ya kukiri kosa na kifungo lakini majadiliano hayo hayakufanikiwa katika dakika za mwisho," Mwanasheria wa Mugabe Sinenhlanhla Mnguni alisema.

Alipuuza semi kuwa Matonhodze anakubali lawama ili kumnusuru Mugabe, akitaja madai hayo "yasiyo ya msingi."

Silaha iliyotumiwa haijapatikana tangu wawili hao walipokamatwa Februari 19.

Kesi iliahirishwa hadi Aprili 24.

Bellarmine ni mmoja kati ya watoto wawili wa kiume ambao Robert Mugabe alipata na mkewe wa pili Grace. Ndugu hao wakati mwingine wamekuwa wakiishi Johannesburg, ambapo wanajulikana kwa kuishi maisha ya kifahari.

Mugabe, ambaye alifariki dunia 2019, alikuwa madarakani kwa miaka 37 kabla ya kuondolewa katika mapinduzi ya 2017.