Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema siku ya Alhamisi kuwa anaelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku kukiwa na mlipuko mwingine wa Ebola.
“Ebola imerudi,” Ghebreyesus alisema katika ujumbe kwenye mtandao wa X. “Nitakuwepo DRC na wahudumu wa WHO, washirika na wahudumu wengine wa afya ambao wamekuwa wakikabiliana na hali muda wote.”
Akiahidi kufanya kila kitu “ndani ya uwezo wake” kusaidia kudhibiti mlipuko huo hatari, aliongeza katika ujumbe mrefu kwa watu wa DRC: “Nataka niwe pamoja na nyinyi kipindi hiki. Na nataka nyinyi mjue kuwa hamko peke yenu.”
Amesema mkoa wa Ituri “umeathirika zaidi” kwa mlipuko huo na kwamba serikali ya DRC imekuwa ikiongoza juhudi za kukabiliana na hali.
Wamefanikiwa mara kumi na sita
Mkuu wa WHO amesisistiza kuwa DRC imefanikiwa kukabiliana na milipuko ya Ebola hapo awali.
“Mara kumi na sita, nchi hii imefanikiwa kudhibiti Ebola. Huu mlipuko wa 17 pia itafanikiwa ,” Tedros amesema. “Lakini lazima tuchukue hatua kwa pamoja sasa.”
Idadi ya maambukizi ya Ebola imepita zaidi ya 1,000 huku yakiongezeka mikoa ya mashariki, kulingana na taarifa ya tathmini ya hali iliotolewa siku ya Jumatano na Wizara ya Afya.


















