Utajiri wa Afrika: Afrika inadai fidia

Umoja wa Afrika umeongeza rasmi ajenda ya kutafuta jinsi ya kulipwa fidia kwa bara kuwa kati ya 2026–2036 na Marais pia wameamuru kuanzishwa kwa mifumo ya kitaasisi ili kuendeleza haki ya ulipaji.

By Coletta Wanjohi
Vitu kadhaa vya sanaa vilirudishwa Ethiopia kutoka Ujerumani baada ya miaka 120 / Reuters

Afrika inataka kile kilichochukuliwa na nchi za Ulaya na Marekani wakati wa ukoloni kirudishwe. Jamii tofauti barani ziliathiriwa.

Ghana iliongoza kwa mafanikio makubwa kuwasilisha hoja ya kuutaka Umoja wa Mataifa kuitambua biashara ya utumwa iliyovuka Atlantiki kama uhalifu.

Huku mahitaji ya malipo ya fidia yakiendelea, baadhi ya vito vya thamani pia vimerudishwa barani humo. Wacha tuangalie uchache:

Ya hivi karibuni zaidi ni kurejeshwa kwa mabaki ya watu takriban 63 kutoka jamii ya Khoi na San ya Afrika Kusini.

Mabaki hayo yalifukuliwa kati ya mwaka 1868 na 1924 na kukabidhiwa Jumba la Makumbusho la Hunterian katika Chuo Kikuu cha Glasgow huko Uskochi.

Kati ya mwaka 2025 na 2026, zaidi ya vito 100 vya shaba vya Benin ambavyo viliporwa kutoka Nigeria mwaka 1897 vilirejeshwa na Uholanzi na Chuo Kikuu cha Cambridge.

Shaba ya Benin ni mkusanyiko wa maelfu ya vyuma na sanamu ambazo zilipamba jumba la kifalme la utawala wa Benin, katika eneo ambalo sasa ni Edo Nigeria.

Mwaka huo huo, Ujerumani iliirudishia Ethiopia vito vya thamani 12 na zaidi ya hati za Kikristu na ngao kutoka mikusanyiko mbalimbali 2023.

Vito hivi vilichukuliwa wakati wanajeshi wa Uingereza walipoiteka Maqdala, mji mkuu wa mfalme wa wakati huo Tewodros kaskazini-magharibi mwa Ethiopia mwaka wa 1868. Vitu hivyo vilipigwa mnada na kuishia katika makumbusho ya Uingereza.

Mwaka 2022, viongozi wa Ubelgiji walirudisha jino la Patrice Lumumba kwa watoto wake. Lumumba aliwahi kuwa kiongozi muhimu katika historia ya ukombozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwaka 2021 Ufaransa ilirudisha vito 26 Benin, pamoja na kiti cha enzi cha Mfalme Ghezo na mabaki kutoka kasri ya Kifalme ya Abomey.

Novemba 2019, pia ilirudisha upanga wa kihistoria wa karne ya 19 wa kiongozi wa Senegal, Omar Saidou Tall, ambaye aliongoza mapambano dhidi ya mkoloni Mfaransa.

Ulikuwa umechukuliwa na vikosi vya Ufaransa mnamo 1893.

Baada ya miaka 124, Chuo Kikuu cha Cambridge kilikabidhi sanamu ya shaba ya jogoo ambayo hapo awali ilikuwa ya falme yenye uwezo ya Benin. Sanamu hiyo iliporwa na wanajeshi wa Uingereza mwaka 1897, na hatimaye ilirejeshwa Oktoba 2021.

Mwaka 2002, Ufaransa ilirudisha mabaki ya mwanamke wa Afrika Kusini, miaka 200 baadaye.

Sarah Baartman alikuwa mwanamke wa Afrika Kusini ambaye alichukuliwa kwa nguvu kutoka nyumbani kwake na kutumika kama onesho la ajabu katika karne ya 19 Ulaya.

Alifariki mwaka 1815, lakini bado mabaki yake yalikuwa yakioneshwa katika majumba ya maonesho.

Ubongo wake, mifupa na viungo vya siri vilibakia kwenye vyumba vya makumbusho ya Paris hadi 1974.

Hii ni mifano michache tu ya utajiri wa Afrika ambayo inatakiwa kurejeshwa.

Umoja wa Afrika umeongeza rasmi ajenda ya kutafuta jinsi ya kulipwa fidia kwa bara kuwa kati ya 2026–2036 na Marais pia wameamuru kuanzishwa kwa mifumo ya kitaasisi ili kuendeleza haki ya ulipaji.