Siku ya Alhamisi Umoja wa Afrika (AU) ulishtumu mashambulizi ya ndege isiyokuwa na rubani ambayo yaliuwa raia mjini Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akiomba kuwe na utulivu miongoni mwa pande zote katika mzozo unaoendelea kwenye kanda na kutoa wito wa kufanyika uchunguzi huru wa tukio hilo.
Katika taarifa, Mahmoud Ali Youssouf, mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, alieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu taarifa kuwa shambulizi la droni mkoa wa Kivu Kaskazini lilisababisha vifo vya raia, ikiwemo mfanyakazi wa shirika la misaada, na kusababisha uharibifu katika eneo la makazi mjini Goma.
Tume “inashtumu vikali mashambulizi yoyote ambayo yanaweka maisha ya raia hatarini pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya misaada, kwa kukiuka sheria ya haki za binadamu ya kimataifa,” taarifa hiyo ilisema.
Siku ya Jumatano, droni ilishambulia jengo la linalotumiwa na mfanyakazi wa shirika la misaada mjini Goma, na kuwaua watu wasiopungua watatu, ikiwemo mfanyakazi wa shirika la UNICEF kutoka Ufaransa.
Umoja wa Afrika umetaka pande zote zinazohusika kwenye mgogoro huo kuwa na utulivu na kujiepusha na hali yoyote ambayo itazidisha taharuki katika kanda. Pia inasisitiza umuhimu wa kuwalinda raia na wafanyakazi wa mashirika ya misaada huko mashariki mwa Congo.
Tume inasema inaunga mkono juhudi za kupata taarifa zaidi kuhusu tukio hilo kupitia uchunguzi huru na kusisitiza umuhimu wa kuheshimu mchakato wa upatanishi na mipango ya kusitisha mapigano wenye lengo la kuleta amani na uthabiti katika eneo hilo la mashariki mwa nchi.
“Umoja wa Afrika bado una dhamira ya kufanya kazi na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, washirika katika kanda, na jamii ya kimataifa kwa lengo la kupata suluhu ya kudumu ya kisiasa, kumaliza uhasama, na kuwa na amani ya kudumu na uthabiti katika kanda,” taarifa hiyo imesema.
Mashariki mwa Congo imekabiliwa na miaka kadhaa ya mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi kadhaa ya waasi.
Katika miezi ya hivi karibuni, mapigano yamezidi kati ya jeshi la DRC na kundi la waasi la M23 mkoa wa Kivu Kaskazini, hasa eneo la Goma, kufanya hali kuwa mbaya zaidi kwa watu na kuzidisha uhasama katika kanda nzima.
M23 inadhibiti eneo kubwa, ikiwemo makao makuu ya mkoa Goma na Bukavu, ambayo walichukua udhibiti mapema 2025.











