Shirika la misaada la Uturuki laanzisha mradi wa ufugaji kuku kwa wanawake wa Tanzania

Shirika la TIKA linalenga kuboresha vipato vya wanawake, na kuwajengea uwezo wa kupata vyenye virutubisho vya protini.

By
Kupitia mradi huo, jumla ya wanawake 30, walipokea mafunzo ya ufugaji kuku pamoja na mbinu za usimamizi wa masoko./Picha:Wengine

Shirika la Maendeleo la Uturuki (TIKA) limezindua mradi wa ufugaji kuku kwa akina mama wa eneo la Tegeta, jijini Dar es Salaam.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na TIKA, mradi huo unalenga kuinua fursa za vipato kwa akina mama hao, pamoja na kuwawezesha akina mama kujipatia vyakula vyenye virutubisho vya protini.

Kupitia mradi huo, jumla ya wanawake 30, walipokea mafunzo ya ufugaji kuku pamoja na mbinu za usimamizi wa masoko.

Baada ya kuhitimisha mafunzo yao, washiriki wa mradi huo walipatiwa bidhaa muhimu kwa ajili ya kuendesha biashara zao.

Shirika hilo, pia lilitoa viatamizi kwa akina mama hao, kama sehemu ya nyenzo muhimu kwa mradi huo.

TIKA, pia ilitoa magari maalumu ya kusambaza mayai, ili kuwapunguzia akina mama hao adha ya kusafirisha bidhaa zao.

Shirika la TIKA limetekeleza jumla ya miradi 350 nchini Tanzania, hasa katika maeneo ya kilimo, ufugaji, elimu, barabara na uwezeshaji wa akina mama.