Malawi itaungana na nchi nyengine kurudisha raia wake walioomba msaada kutoka Afrika Kusini, ambapo wahamiaji wamekuwa wakishambuliwa katika baadhi ya maeneo nchini humo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi imesema katika taarifa yake Jumanne kuwa mpango huo utahusu raia walioomba msaada pekee, na kusema kuwa taarifa zaidi zitatolewa pindi utaratibu kamili utakapokamilika.
Mashambulio dhidi ya raia wa kigeni yamekuwa yakitokea mara kwa mara nchini Afrika Kusini, ambapo raia wa kigeni mara nyingi wamekuwa wakilaumiwa kwa kuchukua ajira za raia.
Makundi yanayopinga kuwepo kwa wageni, yameweka Juni 30, kama siku ya mwisho kwa wageni wote wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria kuondoka, hali inayoongeza wasi wasi katika jamii ya wageni.
Msumbuji imesema raia wake watano wameuawa katika vurugu zilizotokea katika mji wa pwani wa Mossel Bay mwishoni mwa juma, huku Ghana ikiwa tayari imewaondoa mamia wa raia wake wiki iliyopita.
Kwa upande wake, serikali ya Afrika Kusini imeahidi kuwasaka wale wanaochochea vurugu dhidi ya wahamiaji.
Rais Cyril Ramaphosa ameliambia bunge siku ya Jumanne kuwa utatuzi wa tatizo la wahamiaji haramu ni muhimu, lakini nchi haitakiwi kutumia "vurugu dhidi ya wahamiaji."
Afrika Kusini ina uchumi imara katika bara la Afrika na ni kimbilio la wengi wanaotafuta kazi kutoka nchi nyengine.
Pia ni nchi yenye wakimbizi wengi kutoka maeneo yenye migogoro kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.



















