UNICEF imeonya kuwa kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan kunawaweka watoto katika hatari kubwa zaidi
Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, amesema mashambulizi dhidi ya kambi za watu waliokimbia makazi yao, maeneo ya makazi ya kiraia katika eneo la Kordofan inafanana na ile ilioshuhudiwa Darfur.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limeonya kuwa kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan kunawaweka watoto katika hatari kubwa zaidi. Onyo hilo lilitolewa siku ya Jumanne, likieleza kuongezeka kwa mashambulizi katika kambi za wakimbizi na maeneo mengine ya kiraia ndani ya maeneo yenye migogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell, amesema watoto katika eneo la Kordofan wanazidi kuuawa, kujeruhiwa na kufurushwa makazi yao. Pia aliangazia kuwa hali kama hiyo imekuwa ikishuhudiwa kwa muda mrefu katika eneo la Darfur, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa raia.
“Familia zilizokata tamaa nchini Sudan zinatafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi baada ya kukimbia njaa na vurugu. Kulindwa kwao ni wajibu,” Russell alisema katika taarifa.
Kwa mujibu wake, UNICEF inaona “mifumo ile ile ya kutatanisha iliyoshuhudiwa Darfur” sasa ikijirudia katika eneo la Kordofan, huku watoto wakiendelea kuuawa, kujeruhiwa, kuhamishwa na kunyimwa huduma muhimu za msingi wakati mapigano yakizidi.
Shirika hilo lilisema onyo lake lilifuatia shambulio lililoripotiwa la ndege zisizo na rubani kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Kordofan Magharibi siku ya Jumatatu na kusababisha vifo vya watoto 15 na wengine 10 kujeruhiwa, na kusisitiza kuwepo kwa hatari ya raia wanaotafuta hifadhi.
“UNICEF inatoa wito kwa Serikali ya Sudan na pande zote zinazohusika katika mzozo kuwalinda raia, hasa watoto, kukomesha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na maeneo ya kuwahifadhi watu waliohama makazi yao, na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kibinadamu kwa usalama, endelevu na usiozuiliwa kwa wale wanaohitaji kwa kusaidiwa kwa haraka huku mahitaji ya misaada ya kibinadamu yakiongezeka kwa kasi kubwa,” ilisema.
Takwimu kutoka ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa takriban raia 57, wakiwemo watoto 15, waliripotiwa kuuawa kati ya Februari 15 na 16 katika majimbo manne nchini Sudan.
Mnamo Februari 15, shambulio linalodaiwa kutekelezwa na Wanajeshi wa Sudan (SAF) lililenga soko la Al Safiya huko Kordofan Kaskazini, na kusababisha vifo vya raia 28 na wengine 13 kujeruhiwa. Siku iliyofuata, ndege nyingine inayodaiwa kuwa ni ya SAF ilishambulia makazi ya wakimbizi wa ndani huko Kordofan Magharibi, na kuua raia 26, wakiwemo watoto 15.
Kando na mashambulizi hayp, ndege zisizo na rubani zinazoendeshwa na kikosi cha RSF ziliripotiwa kulenga shule mbili za msingi huko Kordofan Kusini na Hospitali ya Al-Mazmoun katika Jimbo la Sennar, ofisi hiyo iliongeza.
Mapigano yameongezeka katika jimbo la Darfur nchini Sudan kati ya SAF na RSF, na vile vile katika maeneo ya Kaskazini, Magharibi Kusini mwa Kordofan, ambako mapigano yameongezeka tangu Oktoba mwaka jana.
Vita kati ya RSF na jeshi la Sudan vimeanza tangu Aprili 2023, kufuatia kuanguka kwa serikali ya mpito.
Mnamo Oktoba 26, vikosi vya RSF vililivamia El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, baada ya kuzingirwa kwa siku 500, na kusababisha watu wengi kuyahama makazi yao na kuwasababishia raia hao uhaba wa chakula.