Fainali za AFCON 2025 zinawakutanisha Simba wawili wale wa Teranga kutoka Afrika Magharibi na wale Milima ya Atlas maeneo ya Kaskazini mwa bara.
Jumapili mtoto hatumwi dukani na atakayeteleza ajuwe kimemramba. Senegal ni ile ya Sadio Mane, yule aliyewahi kuwa pale Anfield na Liverpool, ambaye kwa sasa yuko Al-Nassr pale Saudi Arabia.
Inapokuja suala la kunyanyua ndoo ya AFCON wote Senegal na Morocco wamepata fursa hiyo mara moja tu. Simba wa Teranga ikiwa ni wa AFCON ya hivi karibuni ya 2021 iliyochezwa 2022.
Sasa kwa Morocco mara ya mwisho kushinda ilikuwa hakuna simu janja, hakuna mitandao ya kijamii na hakuna na timu zilizoshiriki wakati huo zilikuwa nane pekee…mwaka 1976. Michuano hiyo ilichezwa nchini Ethiopia.
Timu zote mbili zinajivunia wachezaji wenye uwezo mkubwa na ambao wamecheza katika ligi kuu mbalimbali duniani.
Simba wa Teranga wana Sadio Mane ambaye amecheza katika ligi za Ufaransa, Ujerumani na England na sasa Saudi Arabia. Mwamba huyo amevaa uzi wa timu ya taifa mara 125. Akiwa na umri wa miaka 33 ametikisa nyavu mara 53.
Yuko makini, winga machachari na ni moto wa kuotea mbali.
Simba wa Milima ya Atlas wana Achraf Hakimi pia naye amecheza katika ligi za Ujerumani, Italia, Uhispania na sasa yuko Ufaransa akikipiga na PSG.
Mwamba huyo mwenye umri wa miaka 27 amevaa jezi ya timu ya taifa uwanjani mara 92 na kuifungia magoli 11.
Siku ya Jumamosi Misri itakabiliana na Nigeria kutafuta mshindi wa tatu wa mashindano hayo.
Jumapili utachagua mwenyewe kusuka au kunyoa…itakuwa ni zamu ya Simba wa Teranga kutetemesha tena hatua ya fainali, au Simba wa milima ya Atlas kuchangamsha mashabiki wa nyumbani?


















