Ethiopia inajenga kile kitakachokuja kuwa uwanja mkubwa zaidi wa ndege katika historia ya Afrika. Marekani inasema inataka kuhusishwa katika mradi huo mkubwa. Kwa hiyo, kwa nini Marekani inataka kuhusishwa?
Kazi imeanza katika sehemu ya kupaa na kutuwa ndege ya Uwanja wa Kimataifa wa Bishoftu, ulioko karibu kilomita 45 kusini mashariki mwa Addis Ababa, ilianza mwezi Januari.
Ni mradi wa shirika la ndege la taifa la Ethiopia na unatarajiwa kugharimu dola bilioni 12.5.
Huku kila mtu akitaka kuwa mshirika, Naibu Waziri wa Biashara kuhusu Mashariki ya Kati na Afrika wa Marekani Mark Mitchell anasema Marekani "inawasiliana kwa karibu’’ kwa lengo la kupata fursa ya kushiriki kwenye mradi huo.
Ushawishi wa uwekezaji
Mitchell aliyasema hayo siku ya Jumatano, Julai 29, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya video katika kongamano la Mawasiliano la Afrika lililokuwa lilkifanyika jijini Addis Ababa.
Hakueleza majukumu mahsusi ambayo makampuni ya Marekani yanataka kujihusisha kwenye mradi huo, lakini inasema inaweza "kuuza ndege zaidi aina ya Boeing zinazowezeshwa na GE Aerospace engines".
Hili linakuja wakati Marekani ikishindana na mataifa mengine yenye uwezo kwa ushawishi wa miundombinu na uwekezaji barani Afrika.
Mwezi Januari, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miundombinu na Mipango wa Ethiopian Airlines Abraham Tesfaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa "taasisi za fedha kutoka Mashariki ya Kati, Ulaya, China na Marekani zimeonesha nia ya kuwekeza kwenye mradi huo”
Benki ya Maendeleo ya Afrika pia imeahidi kutoa dola milioni 500 na inaongoza juhudi za kupatikana kwa dola bilioni 8.7.
Mradi huu una umuhimu gani?
Maafisa nchini Ethiopia wanasema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bishoftu utakuwa na eneo la kuegesha ndege 270 na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 110 kwa mwaka utakapokamilika 2030.
Uimarishaji wake ni mara nne zaidi ya uwezo wa sasa wa uwanja mkuu wa Ethiopia jijini Addis Ababa, ambao maafisa wanasema utashindwa kumudu idadi kubwa ya abiria katika kipindi cha miaka miwili au mitatu ijayo.
‘Uwanja mkubwa katika historia’
Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema mwezi Januari kuwa uwanja huo mpya wa ndege ‘’utakuwa mradi mkubwa zaidi katika historia ya Afrika.’’
Viwanja viwili vikubwa kwa sasa barani Afrika kwa idadi ya abiria, ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri na ule wa Afrika Kusini wa O.R. Tambo, vyote vinaweza kuhudumia abiria karibu milioni 30 kila mwaka.
Shirika la Ndege la Ethiopia, ambalo ni kubwa zaidi barani Afrika, lilikubali mwezi Aprili kununua ndege sita zaidi aina ya Boeing 787-9 za Dreamliner kuongeza katika idadi ya ndege 20 ambazo tayari wameagiza. Mapato yake ya mwaka 2025/26 yaliongezeka kwa asilimia 20% hadi kufikia dola bilioni 9.1.
















