Trump asema Rais wa Israel "ni muongo"
Rais Trump amedai kuwa Rais wa Israel Isaac Herzog amemdanganya kuhusu ahadi ya kumsamehe Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa mashtaka ya ufisadi anayokabiliwa nayo.
Rais wa Marekani Donald Trump amemtuhumu vikali Rais wa Israel Isaac Herzog, akidai kuwa ni "dhaifu na wa kukasirisha" na kumshutumu kwa kusema uwongo kuhusu ahadi ya kumsamehe Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
"Aliniambia mara nyingi, zaidi ya mara moja, kwamba atamsamehe, na alinidanganya," Trump aliiambia Channel 14 ya Israel, na kuongeza kuwa Herzog "sio kiongozi."
Alidai kuwa kesi ya Netanyahu inayoendelea ya ufisadi ilikuwa kikwazo katika juhudi za vita.
"Bibi anatakiwa kuangazia vita, sio upuuzi," alisema.
Trump amesisitiza mara kwa mara suala hilo.
Hapo awali alimuita Herzog "mtu dhaifu na asiyefaa" na kumshutumu kwa kutumia suala la msamaha kama ushawishi wa kisiasa.
Afisa mmoja mkuu wa Israel alikashifu matamshi ya Trump, akisema Herzog hajawahi kutoa ahadi kama hiyo na aliwaambia washauri wa Trump kwamba atazingatia ombi hilo kwa kuzingatia taratibu za kisheria.
Netanyahu anakabiliwa na mashtaka ya muda mrefu ya rushwa ya ndani yanayohusiana na upendeleo na manufaa anayodaiwa kupokea badala ya upendeleo wa udhibiti, hatua za kisheria, na msaada wa kidiplomasia kwa wafanyabiashara matajiri na wakubwa wa vyombo vya habari.
Kuhusu vita na Iran, Trump alikataa kufafanua iwapo vikosi vya Marekani vilikusudia kulenga au kukamata miundombinu ya mafuta na gesi ya Iran, akisema tu kwamba hawezi kujibu hilo katika hatua hii.
Mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yalianza Februari 28 na yameripotiwa kuuwa takriban watu 1,300, akiwemo Kiongozi Mkuu wa wakati huo Ayatollah Ali Khamenei.
Iran imelipiza kisasi kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yaliyolenga Israel, Jordan, Iraq na nchi za Ghuba zinazohifadhi mali za kijeshi za Marekani.