Argentina inakabiliwa na msimu wake mbaya zaidi wa maambukizi ya Hantavirus katika miaka ya hivi karibuni, changamoto ambayo sasa imeibua mvutano wa kidiplomasia.
Huku mamlaka za afya nchini zikijitahidi kudhibiti ongezeko hilo ambalo limeshuhudia maambukiiz zaidi ikilinganishwa na mwaka jana, serikali inalilaumu Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa madai ya "kuingiza siasa" katika mlipuko huo.
Kulingana na taarifa ya hivi punde ya mlipuko wa virusi vya Hanta iliyotolewa Jumatatu, Argentina imerekodi maambukizi 101 yaliyothibitishwa katika msimu wa 2025-2026 ulioanza Juni mwaka jana, na hivyo kuashiria ongezeko kutoka maambukizi 57 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.
"Katika nchi nzima, msimu wa mwaka 2025-2026 unaonesha maambukizi kadhaa ambayo yamekuwa juu ya kiwango kwa muda mwingi uliochambuliwa," Wizara ya Afya iliripoti, ikibaini "ongezeko endelevu" ambalo halioneshi dalili za kupungua.
Kufikia sasa katika mwaka wa kalenda wa 2026 pekee, maambukizi 42 yamerekodiwa huku mamlaka ikipambana kutekeleza itifaki za utambuzi wa mapema.
Wataalam wanataja sababu za kimazingira - ukame unaofuatiwa na mvua kubwa - kama kichocheo kikuu cha ongezeko ya maambukizi.
Wakati kipindi cha kiangazi hulazimisha panya katika makazi ya binadamu kutafuta chakula, mvua kubwa huchochea usambazaji wa mbegu, na kusababisha mlipuko miongoni mwa watu.
Wizara ya Afya imehusisha ongezeko hilo pia na "mwingiliano wa binadamu katika mazingira ya mwitu," ikitoa mfano wa uharibifu wa makazi, upanuzi wa makazi ya vijijini, na kuhama kwa maeneo ya ugonjwa unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Virusi vya Hanta vimeibua mzozo wa kisiasa wa kijiografia baada ya kugundulika katika meli ya kitalii ya MV Hondius, ambayo iliondoka kutoka bandari ya Argentina ya Ushuaia Aprili 1.
Machi 2026, Argentina iliifuata Marekani katika kujiondoa rasmi kutoka shirika la WHO. Siku ya Alhamisi, Wizara ya Afya ya Argentina ililishutumu Shirika hilo kwa kutumia maambukizo ya meli "kukosoa uamuzi wake huru" wa kujiondoa kutoka Shirika hilo.
Licha ya msuguano wa kisiasa, maafisa wa afya wanasisitiza kwamba "ufuatiliaji wa kuzuia magonjwa" bado unaendelea.
Hata hivyo, mamlaka bado haijabaini chanzo kamili cha maambukizi ndani ya meli ya MV Hondius.














