Mwakilishi Maalumu wa Jumuiya ya Madola Lazarus Chakwera ahitimisha ziara yake nchini Tanzania
Chakwera ambaye aliwasili nchini humo Aprili 8, 2026 kwa ziara ya kikazi, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola ambaye pia ni Rais wa zamani wa Malawi, Lazarus McCarthy Chakwera ameondoka nchini Aprili 16, 2026, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kuagwa na viongozi waandamizi wa serikali wakiongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mberwa Kairuki, baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku 9 nchini Tanzania.
Chakwera, aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey, Novemba mwaka jana, kuwa mjumbe maalumu wa jumuiya hiyo atakayefanya zaira nchini humo, kuhusu yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Alipokuwa nchini Tanzania, kiongozi huyo alikutana na makundi mbalimbali ya viongozi wa kisiasa, wakiwemo kutoka vyama vya upinzani, na kufanya nao mazungumzo, ambayo hata hivyo yeye mwenyewe hakuyaweka wazi.
Ziara hiyo pia ilimuwezesha kuona maendeleo ya miundombinu ya usafiri Tanzania, ikiwemo safari ya SGR kuelekea Dodoma na usafiri wa boti ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.