Wizara ya Afya ya Kenya imethibitisha kupatikana kwa mgonjwa mwingine aliyeambukizwa ugonjwa wa Ebola, na kufanya jumla ya wagonjwa waliothibitishwa kuambukizwa na ugonjwa huo nchini humo kufikia tisa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo siku ya Jumanne, mgonjwa huyo mpya ni ndugu wa karibu wa mgonjwa wa kwanza aliyegunduliwa kuwa na Ebola nchini Kenya. Mgonjwa huyo alikuwa tayari amewekwa karantini.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini Kenya, Patrick Amoth, alisema wagonjwa wote tisa wameambukizwa na mgonjwa wa kwanza, akieleza kuwa hadi sasa hakuna ushahidi wa ugonjwa huo kuenea zaidi au kutoka kwa mgonjwa mwingine.
“Wagonjwa wote tisa wanahusishwa na chanzo kimoja cha maambukizi, na hadi kufikia leo, hakuna ushahidi wa kuenea kwa maambukizi hayo nje ya kundi hilo,” alisema Amoth katika taarifa yake.
Kenya imeongeza tahadhari kutokana na mlipuko mkubwa wa Ebola unaohusishwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambao umeenea kuvuka mipaka na kuathiri nchi nyingine katika ukanda huo.
Marekani yatoa tahadhari kwa raia wake kuhusu safari za Kenya
Mgonjwa wa kwanza wa Ebola nchini Kenya aligunduliwa mapema mwezi Oktoba. Alikuwa mwanamume aliyesafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hadi Nairobi, ambako baadaye alifariki katika hospitali moja jijini humo Oktoba 5.
Mwishoni mwa Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliwashauri raia wake kutafakari upya mipango ya kusafiri kwenda Kenya kutokana na hatari za kiafya. Aidha, wizara hiyo ilipandisha kiwango cha tahadhari ya usafiri kwa nchi hiyo.
Katika hatua nyingine za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo, Amoth alisema mamlaka za afya zilikuwa zimewafuatilia watu 134 kati ya 135 waliokuwa wamebainika kuwa na mawasiliano na wagonjwa wa Ebola, na kuwaweka karantini hadi kufikia Jumanne.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za mamlaka za afya nchini Kenya za kufuatilia watu walioweza kukutana na wagonjwa na kuzuia maambukizi mapya.






















