Kufunga saum kwa wagonjwa wa Kisukari: Njiapanda kati ya Imani na usalama wa afya
Kwa mujibu wa washauri wa Kitabibu, kufunga wakati wa Ramadhan kunaweza kuendelea kwa njia salama na baadhi ya watu wenye kisukari, lakini uamuzi huo unatakiwa kuwa kwa misingi ya hali ya afya binafsi na ushauri wa kimatibabu.
Mamilioni ya Waislamu wameanza mfungo wa mwezi mmoja, nguzo ya nne ya Imani ya Kiislamu. Na ndivyo inavyotokea sanjari na mfungo wa Wakristo wa Kwaresma na kumaanisha kwamba watu wengi zaidi wanazingatia kwa haraka kwa kipindi hiki.
Hata hivyo pia inazua wasiwasi katika ulimwengu wa matibabu, je, watu wanafahamu miili na afya zao wanapojitahidi kutimiza amri hii ya dini?
Ingawa kufunga ni jambo la hiari katika kipindi cha Kwaresma kwa Wakristo, kwa Waislamu ni desturi ya lazima kwa mtu yeyote aliye katika umri wa baleghe bila shaka kukiwa na udhuru maalum kama, kwa wanawake wajawazito, watu wazima, wagonjwa, wasafiri au hata wanawake walio kwenye siku zao za hedhi.
Baadhi ya misamaha hiyo hukuruhusu tu kuahirisha saumu yako ili kuilipa baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhan pale hali inaporuhusu.
Saumu inawezekana kwa mwenye Kisukari
Lakini ni nini hutokea unapokuwa na ugonjwa kama vile kisukari, ambao huathiriwa sana na si kile unachokula tu bali pia wakati unapokula na nyakati fulani huhitaji kuchomwa sindano za insulini wakati wa mchana?
Kwa mujibu wa washauri wa Kitabibu, kufunga wakati wa Ramadhan kunaweza kuendelea kwa njia salama na baadhi ya watu wenye kisukari, lakini uamuzi huo unatakiwa kuwa kwa misingi ya hali ya afya binafsi na ushauri wa kimatibabu.
Wataalamu wa afya kwa kawaida hutathmini hatari ya mgonjwa kwa kutumia mfumo wa alama ulioidhinishwa ambao huzingatia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa kisukari, aina ya kisukari, na matatizo yoyote yaliyopo.
‘’Watu wenye kisukari walio na viwango vya sukari vilivyodhibitiwa vyema wanaweza kufunga, lakini ni muhimu kushauriana na watoa huduma za afya wiki 6 hadi 8 kabla ya Ramadhan ili kujadili hali ya mtu binafsi na kufanya maamuzi sahihi,’’ anasema Profesa Maïmouna Ndour Mbaye, mkuu wa Madaktari na Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kisukari, Hospitali ya Abass Ndao, Dakar, Senegal.
Madaktari pia wanasisitiza juu ya vipimo sahihi ili kubaini, ikiwa una ugonjwa wa kisukari na haswa ni aina gani ya kuweza kuchukua hatua muhimu za tahadhari wakati wa mfungo wako.
Walio katika hatari kubwa
‘’Wagonjwa wa kisukari aina ya 1 na wale walio na aina ya 2 ambayo haijadhibitiwa vyema kwa ujumla wako katika hatari kubwa zaidi wakati wa kufunga,’’ anaongeza Profesa Maimouna.
Zaidi ya hayo, wanawake wajawazito, watu walio na matatizo kama vile ya moyo na shinikizo la damu au figo au wale wanaotumia insulini pia wako kwenye hatari kubwa na wanahitaji ufuatiliaji wa karibu katika kipindi chote cha kufunga.
Baadhi ya hatari ni pamoja na hypoglycemia (sukari ya chini kwenye damu), hyperglycemia (sukari ya juu ya kwenye damu), na ketoacidosis ya kisukari, upungufu wa maji mwilini, na thrombosis, yaani mgando wa damu kwenye mishipa.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, ikiwa kuna hatari kubwa kwa afya yako unapofunga, basi unaruhusiwa kutofunga. Unaweza kufidia kwa njia nyinginezo kama vile kuwalisha masikini katika mwezi wa Ramadhan.
Lakini kwa waumini wengi walio na kisukari, wajibu wa kutekeleza amri ya dini ya kufunga mara nyingi huzidi tahadhari ya afya yao.
Fuatilia vipimo mara kwa mara
Ili kupunguza hatari Profesa Maimouna anashauri kwamba mtu anatakiwa kuwasiliana na watoa huduma za Afya: angalau miezi 6 hadi 8 kabla ya Ramadhan kutathmini kiwango cha hatari yao na kupata ushauri wa binafsi kulingana na hali yao ya afya.
‘’Pia ni muhimu sana kuangalia viwango vya sukari mwilini mara kwa mara ili kurekebisha ulaji wa chakula na dawa. Wengine wanaweza kuhitaji kubadili muda wa kipimo, kiasi au hata aina ya dawa za kisukari,’’ anaongeza.
Wagonjwa wa kisukari wanaofunga wanatakiwa kuzingatia vyakula vyenye viwango vya chini vya wanga, na vilivyojaa protini wakati wa chakula chao cha alfajiri (Suhoor) na cha kufungua (Iftar) ili kuhakikisha upatikanaji wa nishati kwa mpangilio na endelevu.
Wataalamu wa lishe wanashauri kwamba wagonjwa wa kisukari wanatakiwa kuzingatia aina zifuatazo za vyakula ili kudumisha viwango vya nishati wakati wa kufunga:
- Wanga ulio kamili: Nafaka nzima, kunde, na mboga za wanga ili kutoa nishati endelevu, ambayo hudhibiti viwango vya sukari kwenye damu na kuzuia njaa.
- Vyakula kama: Matunda, mboga mboga na nafaka ili kusaidia kudhibiti pia viwango vya sukari kwenye damu.
- Mafuta yenye Afya: Karanga, mbegu na parachichi zinaweza kutoa virutubisho muhimu huku zikisaidia kuleta usawazishaji wa sukari kwenye damu.
- Protini: Nyama isiyo na mafuta, samaki, mayai, na maziwa inaweza kushibisha na viwango vya nishati.
Shirikisho la Kimataifa la Kisukari (IDF) linaripoti kuwa watu wazima milioni 537, au asilimia 10.5 ya watu duniani, walikuwa wanaishi na ugonjwa wa kisukari kufikia 2021. Idadi hiyo inakadiriwa kufikia milioni 783 ifikapo mwaka 2045.
Lakini karibu nusu ya watu wote wenye ugonjwa wa kisukari hawajui kuwa wanayo. Viwango vya juu zaidi vya wagonjwa ambao hawajatambuliwa ni katika nchi za kipato cha chini na cha kati, hasa Afrika, Pasifiki ya Magharibi na Asia ya Kusini. Kuchelewa kutambua kunaongeza matatizo ya figo, upofu na maradhi ya moyo.
Kati ya Waislamu bilioni 1.9 duniani, karibu asilimia 25 ya watu duniani, takriban watu wazima milioni 150 wanaishi na kisukari, kulingana na Utafiti wa Kisukari na Ramadhan (DAR) 2020 Global.
Hili linaufanya mfungo wa Ramadhan kuwa tatizo kubwa la afya kwa umma.