Wito wa kufanya marekebisho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unasikika tena katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Lakini huu si mjadala mpya. Kwa miongo kadhaa, viongozi wa dunia, hasa kutoka Afrika na mataifa mengine yanayoendelea (Global South), wamesisitiza kuwa chombo kilichoanzishwa zaidi ya miaka 80 iliyopita hakionyeshi tena uhalisia wa dunia kinayoiwakilisha.
Ujumbe huo umesisitizwa mara kwa mara na viongozi wa zamani na wa sasa. "Tumeomba na kuomba na kuomba: fanyeni marekebisho, fanyeni marekebisho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," alisema Hayati Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, katika mojawapo ya hotuba zake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amemalizia hoja yake mara kwa mara kwa kauli moja: "Dunia ni kubwa kuliko mataifa matano."
Na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayemaliza muda wake, António Guterres, naye ametoa wito kwa Baraza hilo kuakisi vyema "dunia ya sasa."
Kiini cha mjadala
Afrika ndiyo kiini cha mjadala huu. Licha ya kuwa na nchi 54 kati ya nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, Afrika haina kiti cha kudumu.
"Afrika lazima ipewe uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiambatana na haki na majukumu yote," alisisitiza Rais wa Ghana, John Mahama, katika kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo tarehe 23 Septemba 2026.
Kwa nini mageuzi yamekuwa magumu sana? Iliyoundwa mwaka wa 1945 wakati Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa, Baraza hilo lina jukumu la msingi la kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
Linaweza kuweka vikwazo, kuanzisha shughuli za kulinda amani na kuidhinisha matumizi ya nguvu.
Leo lina wanachama 15: kumi waliochaguliwa kwa mihula ya miaka miwili na watano wanachama wa kudumu wanaojulikana kama P5 - China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani, ambao wanashikilia madaraka ya kura ya turufu.
Kura ya hapana kutoka kwa mmoja tu inaweza kuzuia azimio. Kurekebisha muundo huu ni vigumu sana.
Chini ya Kifungu cha 108 cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, marekebisho yanahitaji kuidhinishwa na theluthi mbili ya Baraza Kuu na kuidhinishwa na theluthi mbili ya nchi wanachama, ikiwa ni pamoja na wanachama wote watano wa kudumu.
Kwa maneno mengine, wale wanaoombwa kushiriki madaraka lazima wakubali.
Ushindani kati ya P5 ni kikwazo zaidi. Baadhi ya nchi pia zitahitaji kubadilisha sheria za ndani ili kuziwezesha kuidhinisha marekebisho yoyote ya Mkataba, ambayo yanaweza kugumu upanuzi wa Baraza hata kama viongozi watakubali.
Kushiriki mamlaka ya kura ya turufu
Pia kuna kutokubaliana kuhusu ni nani anapaswa kupata viti vipya vya kudumu na kama wanapaswa kuwa na kura ya turufu.
P5 haionekani kuwa tayari kushiriki mamlaka ya kura ya turufu, huku baadhi ya nchi ambazo si wanachama wa kudumu zikitaka ifutwe au kuzuiwa.
Hata hivyo, Afrika inaendelea kusisitiza na kudai angalau viti viwili vya kudumu. India, Brazil, Ujerumani na Japan nazo zimeomba uanachama wa kudumu, huku nchi nyingine zikipendelea kuongezwa kwa viti vya kuchaguliwa pekee.
"Marekebisho ya taasisi hii (Umoja wa Mataifa) lazima yaanzie kwenye uundaji upya wa Baraza la Usalama, kwani dunia ya mwaka 2026 haiwezi kusalia mateka wa mgawanyo wa madaraka wa mwaka 1945. Afrika haiwezi kuendelea kujaza ajenda za baraza hilo huku ikiwa haimo miongoni mwa wanachama wa kudumu," Makamu wa Rais wa Nigeria, Kashim Shettima, aliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mnamo tarehe 24 Septemba 2026.
Nigeria inadai "angalau viti viwili vya kudumu kwa ajili ya Afrika, vikiwa na haki na majukumu yote ya uanachama wa kudumu, ikiwemo haki ya kura ya turufu (veto) ilhali haki hiyo bado ipo—pamoja na jumla ya viti vitano visivyo vya kudumu," alisema Shettima, ambaye alimwakilisha Rais Bola Tinubu.
Baraza hilo liliongeza idadi ya wanachama kutoka 11 hadi 15 mwaka 1965, lakini muundo wake wa wanachama wa kudumu haujabadilika tangu mwaka 1945.
Hivyo, baada ya miongo kadhaa ya wito wa mabadiliko, kikwazo kikuu kinabaki kuwa: unawezaje kugawanya upya madaraka wakati wale wanaoyashikilia wana kauli ya mwisho kuhusu iwapo yagawanywe au la?





















