| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Rais Ruto wa Kenya azungumzia changamoto za bei ya mafuta na gharama za maisha
Rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa nchi haina uhaba wa mafuta licha ya wasiwasi wa kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo, kutatizika kwa usafiri na hofu kuhusu upatikanaji wa mafuta kutokana na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati.
Rais Ruto wa Kenya azungumzia changamoto za bei ya mafuta na gharama za maisha
Rais wa Kenya William Ruto. / Reuters

Rais wa Kenya William Ruto anasema serikali imepata uhakika wa mafuta kupitia mpango wa serikali kwa serikali, akisisitiza kuwa kwa mkataba wao kimataifa wanaouza mafuta wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanapata bidhaa hiyo nchini.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika Ikulu ya Mombasa huku akiangazia tatizo linaloendelea la mafuta, Ruto amesema serikali inafahamu changamoto wanazokabiliana nazo watu za kiuchumi nyumbani, katika biashara na wahudumu wa usafiri wa umma lakini akasisitiza kuwa hali kwa sasa ni shwari.

“Ningependa kuwafahamisha kuwa hakuna uhaba wa mafuta. Kupitia mpango wa serikali kwa serikali, mkataba wetu wa kimataifa tunatakiwa tupate mafuta bila tatizo lolote,” Ruto alisema.

“Serikali inachukua hatua zote kuhakikisha kuwa mafuta yanapatikana."

Rais alikiri kuhusu matatizo ambayo Wakenya wanapitia kufuatia kupanda kwa bei za mafuta, akisema serikali inaelewa changamoto hizo za familia, wafanyakazi na biashara ndogo ndogo kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

“Kwa kila mama ambaye ana wasiwasi kuhusu bei ya vyakula, kila mfanyakazi mwenye wasiwasi kuhusu kama atamudu bei ya nauli akienda kazini kesho, kila mfanyabiashara anayejitahidi kuendeleza biashara yake ndogo, na kila kijana ambaye ana wasiwasi kuhusu mustakabali, nataka mfahamu kuwa serikali ya Kenya inatambua mnayopitia na iko pamoja na nyinyi,” alisema.

Ruto pia alikuwa na ujumbe kwa wahudumu wa usafiri wa umma, wamiliki na wadau katika sekta hiyo ambayo imeathirika pakubwa na kupanda kwa bei ya mafuta.

CHANZO:TRT Afrika Swahili