Iran imetangaza kuwa imelenga kambi za kijeshi za Marekani katika nchi sita za Kiarabu, baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani ndani ya eneo la Iran.
Wakati huohuo, Kuwait, Qatar, Bahrain na Jordan zilisema kuwa ziliyazuia makombora na ndege zisizo na rubani za Iran zilizokuwa zikilenga maeneo yao.
Kikosi cha Walinzi cha Mapinduzi cha Kiislamu cha Iran (IRGC) kilisema siku ya Ijumaa kuwa Kikosi chake cha Anga kililenga kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait, ikiwa ni sehemu ya wimbi la 12 la operesheni yake, kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr.
IRGC ilisema malengo hayo yalijumuisha rada ya kugundua na kufuatilia mifumo ya ulinzi wa makombora, maghala kadhaa ya silaha, vizindua viwili vya mfumo wa makombora ya HIMARS, pamoja na makombora yaliyokuwa yamehifadhiwa kwa ajili ya mfumo huo.
Kikosi hicho kilidai kuwa shambulio hilo lilisababisha moto mkubwa katika kambi hiyo.
IRGC ilisema operesheni hiyo ilifanyika ili kujibu mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani ambayo Iran ilidai yalilenga maeneo ya kiraia, miundombinu ya mawasiliano, wafanyakazi wa reli na magari, na kusababisha vifo na majeruhi.
Kuwait
Jeshi la Kuwait lilisema wanajeshi kadhaa wa nchi hiyo walijeruhiwa baada ya ndege zisizo na rubani za Iran kulenga vituo na kambi kadhaa za kijeshi nchini humo. Jeshi halikutaja idadi ya waliojeruhiwa wala kubainisha maeneo yaliyoshambuliwa.
Awali, jeshi hilo lilisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuzuia makombora na droni za Iran zilizokuwa zikielekezwa dhidi ya nchi hiyo.
Oman
Nchini Oman, IRGC ilisema jeshi lake la wanamaji lililenga maeneo ya rada, ikiwemo rada ya kudhibiti anga ya Marekani, kwa mujibu wa shirika la habari la ISNA.
Likirejea taarifa ya IRGC, ISNA liliripoti kuwa rada ya udhibiti wa majini katika eneo la Salameh Rocks na rada ya Marekani ya kudhibiti anga katika eneo la Ghanem nchini Oman zililengwa alfajiri. IRGC ilidai kuwa mifumo yote miwili iliharibiwa.
Syria
Nchini Syria, IRGC ilisema Kikosi chake cha Anga kilishambulia kituo cha uongozi wa operesheni maalumu cha Marekani katika eneo la Al-Tanf, kwa mujibu wa shirika la habari la Fars.
IRGC ilidai kuwa shambulio hilo liliharibu mfumo wa rada na helikopta kadhaa za operesheni maalumu. Pia ilidai kuwa wanajeshi kadhaa wa Marekani walikamatwa wakati wa operesheni hiyo.
Hakukuwa na ufafanuzi wa haraka kutoka kwa mamlaka za Syria kuhusu madai hayo.
Hata hivyo, chanzo cha kijeshi cha Syria kilikanusha kuwa Iran ililipua kambi hiyo, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
“Tunakanusha madai ya shambulio lolote la Iran dhidi ya eneo la Al-Tanf,” kilisema chanzo hicho bila kutajwa jina. Vikosi vya Marekani vilisema viliondoka katika kambi hiyo mapema mwaka huu.
Jordan
Jordan ilisema ilizuia na kuangusha makombora matatu ya Iran yaliyoingia katika anga yake, huku kukiwa hakuna taarifa za vifo au majeruhi, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Petra.
Wakati huohuo, IRGC ilisema ilifanya mashambulio mawili dhidi ya ndege za kivita za Marekani na ndege za kuongeza mafuta angani zilizokuwa nchini Jordan, kwa kutumia makombora kadhaa ya masafa marefu na idadi kubwa ya droni, kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran (IRNA).
Qatar
Vikosi vya Qatar pia vilisema vilizuia mashambulizi kadhaa ya anga yaliyokuwa yamelenga nchi hiyo, kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Qatar.
Wizara ya Mambo ya Ndani ilisema mtoto mmoja alijeruhiwa na vipande vya mabaki ya makombora baada ya operesheni za kuzuia mashambulizi hayo.
IRGC ilisema ilishambulia Kambi ya Anga ya Marekani ya Al Udeid nchini Qatar, ikidai kuwa iliharibu mfumo wa rada wa masafa marefu na ndege kadhaa za Marekani za kuongeza mafuta angani.
Bahrain
Jeshi la Iran pia lilisema lilifanya shambulio la kutumia droni dhidi ya maeneo yanayotumiwa na ndege za kijeshi za Marekani katika Kambi ya Anga ya Al-Sakhir nchini Bahrain.
Iran ilidai kuwa ililenga maeneo ambako helikopta za kijeshi za Marekani na ndege za doria za baharini na upelelezi aina ya P-8 zilikuwa zimewekwa.
Jeshi la Ulinzi la Bahrain lilisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuzuia na kuharibu “mashambulizi kadhaa ya hila ya anga kutoka Iran.”
Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilisema siku ya Alhamisi kuwa ilikamilisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran, likiwa ni usiku wa sita mfululizo wa operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya mali za kijeshi za Iran, hasa kusini mwa nchi hiyo.
Mvutano wa kikanda umeongezeka katika eneo la Mlango-Bahari wa Hormuz huku Marekani na Iran zikiendelea kushambuliana, licha ya hati ya maelewano yaliyosainiwa mwezi uliopita kwa upatanishi wa Pakistan, yenye lengo la kusitisha mzozo huo na kufikia makubaliano ya kudumu ya amani.



















