Uturuki kuimarisha uwepo wake wa kijeshi kuisaidia Somalia kupambana na ugaidi
Uturuki inaimarisha uwepo wake wa kijeshi huku Somalia ikikabiliana na wimbi jipya la mashambulizi ya kigaidi ya Al-Shabaab.
Taarifa kutoka kwa maafisa wa usalama wa Uturuki zinasema kwamba Uturuki imeongeza uwepo wake wa kijeshi nchini Somalia, ikiwa ni pamoja na kupeleka vitengo vya anga na ardhini vinavyolenga kusaidia taifa hilo la Afrika Mashariki katika mapambano yake dhidi ya ugaidi, huku mashambulizi yakiendelea kuongezeka jijini Mogadishu na mikoa yake jirani.
Kikosi cha Pamoja cha Somalia-Uturuki na Kamandi ya Kitengo cha Anga cha Uturuki vinaendelea kuimarisha uwezo wa Somalia wa kupambana na ugaidi kupitia msaada wa kijeshi, mafunzo, na ushauri wa kitaalamu, wamesema maafisa wa usalama wa Uturuki siku ya Alhamisi.
Kamandi ya Kitengo cha Anga cha Uturuki nchini Somalia imeimarishwa kwa kuongezwa kwa vitengo vipya, na rasilimali mpya zilizowekwa pia zitsaidia katika operesheni za kupambana na ugaidi nchini Somalia, wanasema.
Mapambano ya Somalia dhidi ya Al-Shabaab
Somalia imekuwa ikipigana na Al-Shabaab, kundi la kigaidi linalohusiana na Al-Qaeda, kwa zaidi ya muongo mmoja.
Licha ya shinikizo la kijeshi lililodumu kutoka kwa majeshi ya Somalia, vikosi vya Umoja wa Afrika na washirika wa kimataifa, kundi hili linaendelea kutekeleza mashambulizi ya kigaidi, hasa jijini Mogadishu na mikoa ya jirani.
Miezi ya hivi karibuni, Al-Shabaab imeongeza mashambulizi yake dhidi ya taasisi za serikali, vikosi vya usalama na sehemu zinazokusanya umma, ikionyesha uwezo wa kundi hilo kutumia mapengo ya usalama hata wakati mamlaka ya Somalia ikiendelea na kulishambulia kundli hilo katika maeneo yote ya nchi.
Msaada wa kuendelea wa Uturuki
Uturuki imeibuka kuwa moja ya washirika wa karibu wa usalama wa Somalia, ikiongoza kituo kikubwa cha mafunzo ya kijeshi jijini Mogadishu na kutoa msaada mkubwa kwa Jeshi la Taifa la Somalia.
Maelfu ya wanajeshi wa Somalia wamefundishwa na wakufunzi wa Kituruki, na Uturuki imepeleka vifaa, msaada wa kiufundi na mwongozo wa operesheni.
Maafisa wa Uturuki wanasema lengo ni kusaidia Somalia kujenga mfumo wa usalama unaojitegemea, unaoweza kudumisha utulivu wa muda mrefu na kupunguza utegemezi kwa vikosi vya kigeni.
Kuongezwa hivi karibuni wa nguvu za kijeshi unaashiria nia ya Uturuki ya kuimarisha ushirikiano huo katika wakati muhimu, huku mamlaka ya Somalia ikijaribu kuthibitisha mafanikio dhidi ya Al-Shabaab na kuzuia kundi hilo kurudisha udhibiti wa maeneo.