Wairan wenye uraia wa Marekani wamegawanyika kuhusu ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia, huku baadhi wanapanga kuangalia mechi ya Jumatatu huku wengine wakipanga kuandamana nje ya uwanja ambapo michuano hiyo itafanyika.
Maandamano yamepangwa nje ya uwanja karibu na Los Angeles, makazi ya jamii kubwa ya Wairan wanaoishi jijini humo.
Wengi wao walifika Kusini mwa California wakati wa mapinduzi ya mwaka 1979, na kitovu cha maeneo ya kula, maduka na masoko katika eneo la takriban kilomita 16 kutoka uwanjani linajulikana kama “Tehrangeles.”
Ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia umekumbwa na mgogoro kwa sababu ya vita na Marekani na vikosi vya Israel.
Timu ilihamisha kambi yake ya mafunzo kutoka Tucson, Arizona, hadi Mexico, na baadhi ya maafisa muhimu wa timu wamenyimwa viza ya kuingia nchini Marekani.
Wengi waliopo nje ya nchi wana hisia mchanganyiko kuhusu namna ya kuwaunga mkono raia wenzao, lakini sio serikali, kupitia ushabiki wao kwa mpira.
“Tunawachezea Wairan wote, walio nje ya nchi au nchini Iran. Watu wana maoni tofauti, lakini tuko hapa kuunganisha watu, na tutajaribu kuleta furaha kwa Wairan wote popote wanapoishi," amesema kiongozi wa timu Mehdi Taremi katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili.
“Tuko hapa kuwafurahisha watu wa Iran. Hatuhusiki na siasa. Tuko hapa kucheza soka.”
Reza Garajedaghi, 57, amesema ataiangalia mechi hiyo akiwa pamoja na baba yake mwenye umri wa miaka 96 akiwa San Diego.
Amesema hajanunua tiketi kwa sababu ya bei kuwa kubwa. Lakini amesema anaiunga mkono timu, siassa kando, huku akiheshimu mawazo tofauti yanayotolewa na Wairan waishio nje ya nchi.
“Mimi ni shabiki mkubwa wa soka, na vijana, wanatuwakilisha sote Waajemi, Wairan wote duniani," amesema Garajedaghi, ambae aliondoka nchini Iran alipokuwa na miaka 10.
“Kwangu mimi, haijalishi ni serikali gani iko madarakani."













