Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, amekutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 16, 2026, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia amelishukuru Baraza hilo pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kwa utayari wao wa kufanya mazungumzo na mashauriano ya kuimarisha misingi ya Taifa.
Kulingana na kiongozi huyo, ni wakati mwafaka kwa wadau wa kisiasa kuendeleza mashauriano na wadau wa kisiasa, taasisi za kiraia pamoja na sekta binafsi ili kuunda Tume ya Maridhiano na Upatanishi itakayoratibu maandalizi ya mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Sasa ni wakati mwingine wa kuendeleza mashauriano na wadau wa kisiasa, taasisi za kiraia na sekta binafsi kwa kuunda Tume ya Maridhiano na Upatanishi, itakayoratibu maandalizi ya mchakato wa Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alieleza.
Kwa upande wao, wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa wamependekeza kuundwa kwa Tume ya Maridhiano itakayokuwa na jukumu la kujumuisha na kuzingatia maslahi ya pande zote mbili za Muungano pamoja na usawa wa kijinsia.
Kikao hicho pia kimeendelea na hatua za mashauriano kati ya Rais Samia na wadau mbalimbali kuhusu mchakato wa maridhiano nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia alikutana na wagombea urais pamoja na wagombea wenza wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akiwemo viongozi wa vyama vya siasa.



















