Somalia yazuia ndege ya Israel kupita katika anga yake
Somalia imekataa kuhuisha kibali cha kuruka juu ya anga lake kwa kampuni ya ndege ya Arkia Israeli Airlines, ambayo kwa kawaida hutumia anga la Somalia katika safari zake za moja kwa moja kati ya Tel Aviv na Bangkok.
Serikali ya Shirikisho ya Somalia imekataa kutoa kibali cha kupitisha ndege ya abiria inayomilikiwa na Israel kupitia anga yake, hatua ambayo huenda ikaathiri safari za ndege za kuelekea Asia ya Kusini Mashariki, kufuatia mvutano wa kidiplomasia unaotokana na Israel kulitambua eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland.
Somalia imekataa kuhuisha kibali cha kuruka katika anga yake kwa kampuni ya ndege ya Arkia Israeli Airlines, ambayo kwa kawaida hutumia anga ya Somalia katika safari zake za moja kwa moja kati ya Tel Aviv na Bangkok. Kampuni hiyo imesema bado haijapokea kibali cha kuruka kwa mwezi Februari.
“Hadi sasa, Arkia haijapokea kibali cha mara kwa mara cha kupitisha ndege juu ya anga ya Somalia kwa mwezi Februari,” ilisema kampuni hiyo katika taarifa iliyonukuliwa na vyombo vya habari vya Israel.
Arkia iliongeza kuwa endapo kibali hakitatolewa mapema Februari, italazimika kubadilisha njia ya safari zake za Thailand bila kuathiri ratiba au abiria.
Hatua hiyo inakuja baada ya Somalia kulaani vikali uamuzi wa Israel wa kuitambua Somaliland, eneo la kaskazini mwa Somalia lililojitangazia uhuru mwaka 1991 lakini halijatambuliwa kimataifa.
Serikali ya Somalia imeeleza kuwa Somaliland ni sehemu isiyotenganishwa ya ardhi yake ya mamlaka, na imeutaja uamuzi wa Israel kuwa ni kinyume cha sheria na ukiukaji wa uhuru na mipaka ya Somalia.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Somalia (SCAA), ambayo sasa inadhibiti kikamilifu anga ya nchi hiyo, imekataa ombi la Arkia la kuruka juu ya anga la Somalia.
Uamuzi huo unakuja wakati Somalia ikiimarisha udhibiti wake wa anga ya kitaifa baada ya miongo kadhaa ya kusimamiwa na taasisi za nje.
Arkia imesema suala hilo linashughulikiwa na mamlaka za Israel, zikiwemo Mamlaka ya Usafiri wa Anga na Wizara ya Mambo ya Nje.
Mwaka 2017, serikali ya Somalia ilitangaza kurejesha rasmi udhibiti na usimamizi kamili wa anga yake baada ya zaidi ya miaka 27, ambapo awali anga ya Somalia ilisimamiwa kutoka Nairobi chini ya mpango ulioongozwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga la Umoja wa Mataifa (ICAO), kufuatia kuporomoka kwa serikali kuu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kubadilishwa kwa njia za ndege kunaweza kuwa na athari za kiuchumi. Arkia hivi karibuni ilianzisha safari ya moja kwa moja kati ya Tel Aviv na Bangkok, wakati Thailand ikishuhudia ongezeko kubwa la watalii kutoka Israel.
Mamlaka ya Utalii ya Thailand imeripoti kuwa zaidi ya watalii 400,000 kutoka Israel walitarajiwa kufika nchini humo ifikapo mwisho wa mwaka 2025, huku mapato ya utalii yakikadiriwa kuzidi baht bilioni 34 (sawa na dola milioni 950 za kimarekani).
Hadi sasa, Somalia haijatoa tamko rasmi iwapo kukataa kibali cha kupitisha ndege ni kwa muda au inahusiana moja kwa moja na mzozo wa Somaliland.