Mamlaka nchini Uganda zimeagiza kufungwa kwa mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo “mara moja” huku maambukizi ya aina ya sasa ya Ebola yakiongezeka kwa jirani zao na maambukizi yakiibuka nchini mwao.
Uamuzi huu ulifikiwa na kikosi kazi cha Ebola kinachoongozwa na Makamu wa Rais Jesca Alupo baada ya idadi ya wahudumu wa afya kuongezeka kupata maambukizi ya Ebola kutokana na kutangamana na wagonjwa kutoka DRC waliovuka mpaka kabla mlipuko huo kutangazwa Mei 15.
Uganda imeripoti maambukizi saba ya Ebola, ikiwemo yale ya kwanza ya mwanamume mwenye umri 59 aliyefariki mji mkuu wa Kampala, Mei 14.
Lakini wakati maambukizi ya Ebola nchini Uganda yakiwa hayaongezeki kwa kasi, idadi ya watu wanaotangamana na wale walioambukizwa kupitia wahudumu wa afya inaongezeka.
'Idadi inaongezeka'
“Hawa watu wana familia, kwa hiyo idadi inaongezeka,” Dkt. Diana Atwine, katibu mkuu katika wizara ya afya, alisema kuhusu wahudumu wa afya.
Idadi ya wanaoaminika kuwa na maambukizi ya Ebola mashariki kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefikia 1,000, huku kukiwa na vifo visivyopungua 220.














