Rias wa Senegal Rais Bassirou Diomaye Faye amemteua mwanauchumi Ahmadou Al Aminou Lo kuwa Waziri Mkuu mpya, akisema ana uzoefu unaohitajika kukabiliana na mgogoro wa deni la taifa.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Faye mwezi Mei kumtimua Sonko katika nafasi ya uwaziri mkuu, jambo lililodhihirisha mpasuko mkubwa unaoendelea kati ya viongozi hao wawili ambao hapo awali waliongoza pamoja harakati za upinzani nchini humo.
Sonko alianzisha chama cha PASTEF mwaka 2014 na alichangia kwa kiasi kikubwa kupanda kwa Faye hadi kuwa Rais. Baada ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2024, Faye alimchagua Sonko kuwa Waziri Mkuu, lakini baadaye tofauti zao zilianza kujitokeza kuhusu mwelekeo wa kisiasa na namna ya kushughulikia changamoto za kiuchumi za Senegal.
Kwa upande wake, Sonko ametangaza kuwa chama cha PASTEF hakitashiriki katika serikali mpya, akieleza kuwa bado kuna tofauti kubwa kati yake na Rais.
Licha ya kuondolewa katika nafasi ya waziri mkuu, Sonko bado ana ushawishi mkubwa kisiasa. Hivi karibuni alichaguliwa kuwa Spika wa bunge na anaendelea kuongoza chama cha PASTEF, chama chenye viti 130 kati ya 165 bungeni. Hali hiyo inampa uwezo mkubwa wa kusimamisha na hata kuzuia baadhi ya mipango ya serikali ya Faye.
Mgogoro huu unatokea wakati Senegal ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.
Deni la taifa limefikia takriban asilimia 132 ya pato la taifa (GDP) baada ya kubainika kuwa madeni ya awali yalikuwa yameripotiwa chini ya kiwango halisi.
Kutokana na hali hiyo, Shirika la Fedha la Kimataifa lilisimamisha mpango wake wa mkopo wa Dola bilioni 1.8 kwa Senegal. Wachambuzi wanaonya kuwa mvutano kati ya Faye na Sonko unaweza kufanya mazungumzo yajayo na Shirika la Fedha la Kimataifa kuwa magumu zaidi na kuchelewesha mageuzi muhimu ya kiuchumi.






















