Kenya na Uingereza siku ya Jumanne walikubaliana kuanza tena mazoezi ya kijeshi katika taifa hilo la Afrika Mashariki baada ya kuchelewa kutia saini makubaliano mapya ya kijeshi ambayo yalitokana na wabunge wa Kenya kueleza wasiwasi wao kuhusu kulinda jamii za karibu na eneo la mazoezi na kutaka hakikisho kuwa mpango huo wa BATUK utashughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu.
Serikali zote hazijazungumzia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na wanajeshi wa Uingereza waliohusika katika mazoezi ya awali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alisema serikali imeridhishwa na uamuzi wa kuendelea na mazoezi baada ya ushirikiano uliojengwa kwa misingi “ya kuheshimiana, makubaliano yenye tija, na dhamira ya pamoja kuhusu amani na usalama.”
Kuahirishwa kwa mazoezi hayo kulitangazwa Julai 23. Mamlaka za nchini Kenya zimekanusha taarifa za vyombo vya habari kuwa Uingereza ilikuwa inatafakari kuhamisha mazoezi hayo hadi nchi jirani ya Tanzania.
Kifo cha mwanamke raia wa Kenya
Katika taarifa serikali ya Uingereza ilisema serikali ya Kenya imekubali kutoa leseni husika na idhini na kwamba mazoezi yataanza tena baadaye mwaka huu.
Uingereza ina karibu maafisa 200 wa kijeshi ambao wana makazi yao Kenya na hutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Kenya zaidi ya 1,000 kila mwaka kabla ya kuelekea nchi jirani ya Somalia kukabiliana na kundi la kigaidi la Al Shabab, washirika wa Al Qaeda Afrika Mashariki.
Serikali ya Uingereza inawekeza zaidi ya shilingi bilioni 1.1 ($9.6 milioni) kila mwaka katika ushirikiano huo.
Lakini shinikizo lilizidi kwa uwepo wa Uingereza baada ya mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 21 Agnes Wanjiru kupatikana katika shimo la majitaka mjini Nanyuki, karibu na kambi ya jeshi la Uingereza mwaka 2012, wiki chache baada ya walioshuhudia kusema walimuona akitoka baa akiwa pamoja na wanajeshi wa Uingereza.
Mwaka 2021, moto mkubwa ulioanzishwa na wanajeshi wa Uingereza uliharibu zaidi ya ekari 12,000 za eneo la hifadhi la Lolldaiga karibu na sehemu ya mazoezi.



















