Israel inataka kufuta vibali vya mashirika ya misaada Gaza na Ukingo wa Magharibi

Israel inalenga mashirika ya misaada kuwafutia vibali, ikiyashutumu makundi hayo kwa kushindwa kutimiza masharti ya usajili.

By
Israel kufungia mashirika 37 ya misaada ndani ya Gaza na West bank / Reuters

Serikali ya Israel imeanza kuondoa vibali kutoka kwa mashirika ya kimataifa ya misaada yanayofanya kazi Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikitaja madai ya kushindwa kukamilisha taratibu zinazohitajika za usajili.

Mamlaka za Israel zilisema zinapanga kufuta leseni za mashirika 37 ya misaada, ikiwa ni pamoja na Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), na ActionAid.

Serikali ilidai kuwa baadhi ya mashirika hayo yanawaajiri Wapalestina wanaojihusisha na kile ilichokiita "shughuli za kigaidi."

Kwa mujibu wa gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth, mamlaka tayari imetuma taarifa kwa zaidi ya mashirika 12 ya kimataifa ya misaada kuwafahamisha kwamba vibali vyao vya kufanya kazi huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu vitafutwa kuanzia Januari 1, huku shughuli zote zikitakiwa kusitishwa ifikapo Machi 1.

Maafisa wa Israel walidai kuwa baadhi ya mashirika yalikataa kuwasilisha orodha kamili za wafanyakazi wa Kipalestina kwa kile walichoeleza kuwa uchunguzi wa usalama.

Onyesha orodha ya wafanyakazi au uondoke

Hatua hiyo inaongozwa na timu ya pamoja ya mawaziri chini ya Wizara ya Masuala ya Diaspora na Kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi, ambayo ilituma barua rasmi kwa mashirika yaliyoathiriwa.

Vyombo vya habari vya Israel hapo awali viliripoti kwamba serikali inataka kuweka udhibiti mkali zaidi kwa mashirika ya kimataifa ya misaada yanayofanya kazi huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kupitia utaratibu mpya ambao utayalazimisha kuchagua kati ya kulinda wafanyakazi wao na kuendelea kutoa huduma muhimu.

Ripoti zilisema hatua hizo, ingawa zimeandaliwa kama za kiutawala, zinaonyesha tishio la kuwepo kwa mashirika kadhaa ya kimataifa ambayo yamefanya kazi katika maeneo yanayokaliwa kwa miongo kadhaa.

Israel imeyataka mashirika kuwasilisha orodha ya wafanyakazi wote, wakiwemo Wapalestina, na kuonya kwamba shirika lolote linaloshutumiwa kwa "kukosa uhalali" Israel au kuajiri watu waliounga mkono kususia kazi katika miaka saba iliyopita linaweza kuzuiwa kufanya kazi.

Maafisa wa Israel wamechukua hatua sawa dhidi ya shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, huku bunge la Knesset likiidhinisha sheria mwaka 2024 inayopiga marufuku shughuli zake nchini Israel, hatua ambayo shirika hilo liliikataa, likisisitiza kutoegemea upande wowote.