Wanyonyi azima mahanjam za Mandonga ulingoni
Mandonga 'mtu kazi' sasa anataka pigano jingine dhidi ya Wanyonyi baada ya kupokea kichapo kisichosahaulika na kushindwa kwa pointi licha ya kutua Nairobi kwa mpigo na ngumi yake mpya ya 'Kinguki'.
Bondia maarufu wa Tanzania Karim Mandonga hatimaye amepata pigo lake la kwanza nchini Kenya baada ya Mkenya Daniel Wanyonyi al maarufu 'mwana wefwe' kumpa dozi za 'ngumi dusra' yaani 'ngumi nzito' katika pigano lao la marudio lililofanyika mjini Nairobi.
Wanyonyi, alifanikiwa kulipiza kisasi dhidi ya Mandonga kwa kumtwanga katika pambano lao la marudio baada ya kupoteza mchezo wao wa awali mwezi Januari mwaka huu.
Bingwa huyo wa zamani wa Shirikisho la Ngumi barani Afrika (ABU), Wanyonyi, alifanikiwa kumshinda Mandonga kwa wingi wa alama katika pigano la wawili hao lililoandaliwa na 'Ultrafight series promotions,' katika jengo la Sarit, jijini Nairobi.
Waziri wa Michezo nchini Kenya Ababu Namwamba, alikuwa miongoni mwa mashabiki waliompongeza Wanyonyi kufuatia ushindi wake wa kulipiza kisasi dhidi ya mandonga.
Ingawa pambano hilo lao la ndondi la ubingwa la uzani wa kati halikuwa na taji, lilishuhudia mchuano wenye mvuto
Mashabiki wa Ndondi wanasubiri kwa hamu kuona iwapo Wanyonyi na Mandonga wataingia ulingoni kupigania taji rasmi la shirikisho la ndondi Afrika.