Polisi nchini Afrika Kusini wametoa zawadi ya fedha kwa yoyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wale waliohusika na msururu wa mauaji eneo la Ekurhuleni, mashariki mwa jiji la Johannesburg.
Polisi walipata miili tisa siku ya Alhamisi, na kuzua hofu kuhusu mauaji hayo. Kufikia sasa, miili mitatu imeshatambuliwa.
Zawadi ya tuzo ya R400,000 ($24.600) ilitangazwa wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu njia za kuwakamata wahusika, huku polisi wakiendelea na uchunguzi kuhusu vifo vya wanawake ambao miili yao imekuwa ikipatikana katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili.
Mamlaka zinasema kuwa zinafanya msako mkubwa kuwatafuta wale waliohusika, lakini zimeonya dhidi ya kuunganisha kesi hiyo na zingine hadi pale uchunguzi utakapokamilika.
Kaimu Waziri wa Masuala ya Polisi Firoz Cachalia anasema, “serikali inalipa kipaumbele suala hili. Rais ametangaza tukio hilo kuwa mkasa wa kitaifa, na naweza kusema kuwa mawaziri wanaongoza juhudi za suala hili, na kwa mipango mbalimbali, ikiwemo juhudi za Polisi wa Afrika Kusini, kila jitihada zinafanyika kukabiliana na tukio hili baya.”





















