| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Mapipa milioni 400 ya mafuta kutoka akiba ya dharura kuokoa hali ya uhaba duniani
Wanachama wa IEA wana hifadhi ya dharura ya zaidi ya mapipa bilioni 1.2 na mapipa milioni 600 zaidi ya hisa ya viwanda yakiwa chini ya wajibu wa serikali.
Mapipa milioni 400 ya mafuta kutoka akiba ya dharura kuokoa hali ya uhaba duniani
Wanachama wa IEA wana hifadhi ya dharura ya zaidi ya mapipa bilioni 1.2 ya mafuta / AP
tokea masaa 4

Nchi 32 Wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati, IEA, walikubaliana kwa kauli moja 11 Machi 2026 kutoa mapipa milioni 400 ya mafuta katika hifadhi zao za dharura ili kukabiliana na hali ya uhaba wa mafuta uliojitokeza kufuatia mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

IEA ni shirika la kiserikali lililoanzishwa mwaka wa 1974, ambalo hutoa mapendekezo ya sera, uchambuzi na data kuhusu sekta ya nishati duniani.

Nchi 32 wanachama na nchi 13 za jumuiya ya IEA zinawakilisha 75% ya mahitaji ya nishati duniani.

Uamuzi wa kuchukua hatua za pamoja za dharura ulifanywa kufuatia mkutano usio wa kawaida wa serikali wanachama wa IEA, ulioitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa IEA kutathmini hali ya soko huku kukiwa na mzozo wa Mashariki ya Kati na kuzingatia chaguzi za kushughulikia usumbufu wa usambazaji.

"Changamoto za soko la mafuta tunazokabiliana nazo ni kubwa mno, kwa hivyo ninafuraha sana kwamba nchi Wanachama wa IEA zimejibu kwa hatua ya dharura ya pamoja ya ukubwa ambao haujawahi kushuhudiwa," Mkurugenzi Mtendaji wa IEA Fatih Birol alisema.

"Masoko ya mafuta ni ya kimataifa kwa hivyo mwitikio wa usumbufu mkubwa unahitaji kuwa wa kimataifa pia. Usalama wa nishati ndio jukumu la msingi la IEA, na ninafurahi kwamba Wanachama wa IEA wanaonesha mshikamano mkubwa katika kuchukua hatua madhubuti pamoja."

IEA inasema hisa za dharura zitapatikana sokoni kwa muda unaolingana na hali ya kitaifa ya kila nchi Wanachama na zitaongezewa hatua za dharura na baadhi ya nchi.

Wanachama wa IEA wana hifadhi ya dharura ya zaidi ya mapipa bilioni 1.2 ya mafuta, na mapipa milioni 600 zaidi yakiwa akiba yaliyoshikiliwa na seriklai husika kwa ajili ya matumizi yao wenyewe.

Katika historia ya IEA, hili ni toleo la sita la akiba lililoratibiwa tangu Shirika lilipoundwa mwaka wa 1974.

Hatua za awali za pamoja zilichukuliwa mwaka wa 1991, 2005, 2011, na mara mbili mwaka wa 2022.

Mzozo wa Mashariki ya Kati ulioanza tarehe 28 Februari 2026 umezuia mtiririko wa mafuta kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz, na usafirishaji wa bidhaa ghafi na zilizosafishwa kwa sasa chini ya 10% ya viwango vya kabla ya migogoro.

Hii inawalazimu waendeshaji katika eneo lote kufunga au kupunguza kiasi kikubwa cha uzalishaji.

Wastani wa mapipa milioni 20 kwa siku ya mafuta ghafi na bidhaa za mafuta zikivuka Mlango-Bahari wa Hormuz mwaka wa 2025, au karibu 25% ya biashara ya mafuta ya baharini duniani.

CHANZO:TRT Swahili