Matetemeko ya ardhi ya Uturuki 2023 yalisababisha hasara ya dola bilioni 250: Erdogan
Rais wa Uturuki amesema ndani ya miaka mitatu miji iliyoathiriwa imejengwa upya na kuimarishwa.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa matetemeko ya ardhi yaliyotokea katika mikoa ya kusini na mashariki ya Uturuki mnamo Februari 6, 2023, yalisababisha hasara ya moja kwa moja ya kiuchumi ya dola bilioni 104 na hasara isiyo ya moja kwa moja ya dola bilioni 150, akayaita “moja ya maafa mabaya zaidi katika historia yetu.”
“Kwa kuonyesha mfano bora wa mshikamano kati ya taifa na serikali, tumeponya pamoja vidonda vilivyotokana na tetemeko la ardhi,” amesema Rais Erdogan, akiongeza kuwa Uturuki “imeionesha kwa mara nyingine dunia nguvu zake.”
Akikataa shutuma juu ya jinsi serikali ilivyoshughulikia tetemeko hilo, Erdogan alisema mamlaka “hayakuathirika na siasa chafu zilizo jaribu kutushinikiza na kuvunja uthabiti wetu,” akidai kuwa ndani ya miaka mitatu miji iliyoharibiwa imejengwa upya na kurudi katika hali yake ya kawaida.
Kulingana na Ofisi ya Mikakati na Bajeti ya Uturuki (SBB), nchi hiyo imetumia lira trilioni 3.6 za Uturuki (takriban dola bilioni 91.5 za Marekani) katika jitihada za ujengaji upya ndani ya miaka mitatu iliyopita, huku Kahramanmaras na Hatay zikichukuliwa kuwa kitovu cha ujengaji upya.
Makazi yalipatiwa kipaumbele, na nyumba 433,667 na sehemu 21,690 za kazi ziligawanywa kupitia bahati nasibu, huku ujenzi wa makazi ya kudumu ukikamilika.
Mabillioni ya pesa pia imetumika kwenye elimu, afya, miundombinu, nishati, usafirishaji na msaada wa ajira katika mikoa 11.
Ofisi ya SBB imesema kuwa ujengaji upya umekamilika kwa kiwango kikubwa baada ya jitihada za muda mrefu na za kina, na maendeleo makubwa yamefikiwa katika kurejesha huduma za umma, shughuli za kiuchumi, na maisha ya kijamii katika eneo lililoathiriwa na tetemeko la ardhi.