“Mauaji ya Wakristo”: Kwa nini madai ya Trump kuhusu Nigeria ni yenye upotoshaji na hatari
Madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba kuna “mauaji ya halaiki dhidi ya Wakristo” nchini Nigeria yanapotosha uhalisia wa mzozo unaochochewa na migogoro ya rasilimali, yanahatarisha uhusiano na mshirika muhimu katika vita dhidi ya ugaidi.
Na Emmanuel Oduor
Wakati Trump alipoandika kwenye mtandao wa Truth Social kwamba alikuwa ameagiza Wizara ya Ulinzi kujiandaa kwa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Nigeria, maafisa mjini Abuja walishangazwa.
Madai yake: Taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika linakubali “mauaji ya halaiki dhidi ya Wakristo”.
Serikali ya Rais Bola Tinubu ilikanusha mara moja madai hayo, ikiyaita ya uongo. Hata hivyo, kauli hiyo ya Trump ilisababisha taharuki kubwa ya kidiplomasia, hasa baada ya kulitangaza rasmi taifa la Nigeria kuwa “Nchi yenye kuwatia wasiwasi” kutokana na madai ya ukiukaji mkubwa wa uhuru wa kidini.
Madai ya utawala wa Trump yanaendana na shinikizo kutoka kwa makundi ya waumini wa Kiinjili nchini Marekani na wabunge fulani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka maafisa wa Nigeria wachukuliwe hatua wakidai wamefumbia macho “mauaji ya Wakristo”.
Lakini ukweli ni upi unaofichwa na “Truth Social” ya Trump?
Nchi ya Nigeria yenye watu takribani milioni 220 ina idadi karibu sawa kati ya Wakristo na Waislamu — Waislamu wakiwa zaidi kaskazini na Wakristo kusini.
Upotoshaji wa Ukweli
Kwa miaka mingi, Nigeria imekumbwa na migogoro ya silaha katika maeneo ya kati na kaskazini. Jeshi linapambana na makundi ya kigaidi na magenge ya uhalifu hasa kaskazini mashariki na magharibi mwa kaskazini — maeneo ambayo yana Waislamu wengi.
Hivyo basi, mara nyingi waathirika wakuu wa mashambulizi hayo ni Waislamu.
Trump hakueleza ni mauaji gani aliyokuwa akimaanisha, lakini madai yake kuhusu “mauaji ya Wakristo” yanaonekana kujikita zaidi kwenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Nigeria ya kati.
Wataalamu wa usalama wanasema vurugu hizo kimsingi zinahusu upatikanaji wa rasilimali — ardhi yenye rotuba na madini muhimu kama dhahabu na lithiamu — na kwamba wanaoathirika ni Wakristo na Waislamu kwa kiwango sawa.
Kupinga kauli za kisiasa
Wataalamu wanatahadharisha kuwa kauli ya Trump inaifanya tatizo tata la usalama kuonekena lepesi na inaweza kuongeza mgawanyiko na hali ya kutokuwa na utulivu nchini Nigeria.
Wanasiasa wa Nigeria kutoka pande zote wanakubaliana kuwa mtazamo wa Trump ni wa upotoshaji na unaweza kusababisha hasara kwa pande zote.
Tishio lake la kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Nigeria pia linahatarisha ushirikiano na moja ya uchumi mkubwa zaidi barani Afrika — na mshirika muhimu katika vita dhidi ya ugaidi kwenye ukanda wa Sahel.
“Kadri tunavyoendeleza kauli kama hizi, ndivyo tunavyowapa magaidi nguvu zaidi, na Marekani pamoja na washirika wake watapoteza marafiki wa kushirikiana nao katika vita dhidi ya ugaidi,” anasema mchambuzi wa kisiasa wa Nigeria, Bulama Bukarti, akizungumza na TRT Afrika.
Changamoto zinazoendelea
Baada ya tishio la Trump, Rais Tinubu alisema serikali yake iko tayari kushirikiana na washirika wa kimataifa kutatua changamoto za usalama.
Hata hivyo, wataalamu wanasema hali ni ngumu — vurugu zimekuwa zikijirudia kwa miongo miwili, na jeshi limezidiwa kutokana na mapambano katika maeneo mengi.
Jeshi la Nigeria linapambana na Boko Haram kaskazini mashariki, makundi yanayohusiana na Al Qaeda kaskazini magharibi, na magenge ya majambazi katikati mwa nchi.
Idadi ya wanajeshi haijaongezeka kulingana na ukubwa wa changamoto, huku polisi wakiwa wachache na wasio na vifaa vya kutosha.
“Jeshi la Nigeria bado halina vifaa vya kisasa, silaha, wala uwezo wa kijasusi wa kutosha,” asema Bukarti.
“Pia kuna upungufu mkubwa wa ushirikiano kati ya taasisi nyingi za usalama, zaidi ya taasisi 17, ambazo zote zina jukumu katika kurejesha amani.”
Hofu ya kukabiliana na Trump
Kutajwa kama nchi yenye inayowapa Marekani wasiwasi ni pigo kubwa kwa Nigeria, na linaweza kuwa na athari mbaya zaidi kwa uchumi wake ambao tayari uko katika hali mbaya.
Wataalamu wanasema kurekebisha uhusiano na serikali ya Trump kutahitaji Abuja kuchukua hatua za kidiplomasia kwa utulivu.
“Serikali ya Nigeria inapaswa kuwa na busara, isiingie kwenye malumbano ya maneno. Ni bora ijihusishe kidiplomasia na Marekani, ionyeshe kwamba Waislamu na Wakristo wote ni waathirika wa vurugu, na iombe ushirikiano katika silaha, mafunzo na ujasusi,” asema Bukarti.
Msemaji wa Rais wa Nigeria ameeleza kuwa madai ya Trump yalikuwa “mawasiliano yaliyopotoshwa”, akitumaini kuwa viongozi wa mataifa hayo mawili wataweza “kutatua tofauti zao”.
Mtazamo wa kibiashara wa Trump
Utawala wa Trump umekuwa ukifanya makubaliano na baadhi ya nchi za Afrika kukubali wahamiaji waliorejeshwa kutoka nchi zingine katika juhudi za kudhibiti uhamiaji haramu.
Ghana, Eswatini, Rwanda na Sudan Kusini zimepokea wahamiaji hao, huku Uganda ikikubali makubaliano lakini bado haijampokea yeyote.
Nigeria ilikataa kushiriki katika mpango huo, jambo ambalo wachambuzi wanalihusisha na kupotea kwa uhusiano mzuri kati yake na utawala wa Trump.
Wataalamu wanasema mtindo huu wa “diplomasia ya kibiashara” unalenga kuwashinikiza viongozi wa Afrika, mbinu ambayo Trump pia aliitumia dhidi ya Afrika Kusini kwa madai ya “mauaji ya wazungu”, madai ambayo serikali ya Pretoria imeyakanusha kama ya uongo.