Sagal Abdi-Wali ni mwanamke wa kwanza aliyezaliwa nchini Somalia na kuchaguliwa kuwa mbunge nchini Uingereza.
Safari yake kutoka maisha ya ukimbizi hadi uongozi wa kisiasa katika taifa hilo la kaskazini magharibi mwa Ulaya ni ya kutia moyo.
Alizaliwa Somalia na kufika Uingereza akiwa na umri wa miaka saba pamoja na familia yake, wakiwa wamekimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vinaendelea nchini Somalia.
Alikulia Camden, jijini London, ambako alianza kujihusisha na shughuli za kijamii kabla ya kuingia katika siasa.
Mwaka 2022, alichaguliwa kuwa diwani wa Camden, na Mei 2026 akawa kiongozi wa Halmashauri hiyo ilioko kaskazini mwa mji mkuu wa Uingereza.
Oktoba 2026, alichaguliwa kuwa mbunge wa chama cha Labour katika jimbo la Holborn and St Pancras, akipata asilimia 45 ya kura na kumshinda kiongozi wa Green Party, Zack Polanski, aliyeambulia asilimia 33.
Uchaguzi huo ulifanyika baada ya kujiuzulu kwa Keir Starmer katika nafasi hiyo. Starmer alikuwa mbunge wa eneo hilo kuanzia Mei 2015 hadi Septemba 2026, kwa takribani miaka 11.
Katika kipindi hicho, aliwahi pia kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa miaka miwili kuanzia Julai 2024.
Akiwa katika siasa, Sagal Abdi-Wali amejikita zaidi kwenye masuala ya makazi bora, kupambana na ukosefu wa makazi na kuongeza fursa kwa vijana.
Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 42, katika hotuba yake ya ushindi alisisitiza kuwa watu kama yeye pia wanajivunia kuwa Uingereza ni kwao, akikamilisha kwa kusema ‘’Hii ni Camden na hii ni England.’’
Alikula kiapo rasmi kwa kushika Qur'an pale Westminster siku ya Jumatatu tarehe 12 Oktoba.
















