| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Hamas haipaswi kuondoka kisiasa: Balozi wa Bodi ya Amani
Nickolay Mladenov anasema kundi la upinzani la Palestina la Hamas linaweza kubaki kama kundi la kisiasa, lakini makundi yenye silaha lazima yaweke silaha chini.
Hamas haipaswi kuondoka kisiasa: Balozi wa Bodi ya Amani
Nickolay Mladenov akizungumza na waandishi wa habari Jerusalem Mashariki inayokaliwa kwa mabavu, Jumatano, Mei 13, 2026. / AP

Nickolay Mladenov amesema kundi la Palestina la Hamas linaweza kubaki kisiasa, lakini makundi yenye silaha sharti yaweke silaha chini kutokana na makubaliano ya usitishaji wa mapigano wa Gaza.

Nickolay Mladenov, mjumbe maalumu wa Bodi ya Amani anayesimamia usitishaji wa mapigano Gaza, amesema kwamba Bodi hiyo haitaki kuipoteza Hamas 'kisiasa.'

Akizungumza Jumatano katika mkutano Jerusalam Mashariki iliyokaliwa kwa mabavu, Mladenov amesema “hatutaki Hamas ipotee kama kundi la kisiasa.”

Lakini amerudia madai ya kutaka Hamas na makundi mengine kuweka silaha chini, akilielezea suala hilo kwamba "halina mjadala."

Miezi saba baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza Oktoba 2025, "mlango wa mustakbali wa Gaza bado umefungwa," amesema.

“Sicho walichoahidiwa Wapalestina na sicho wanachostahiki. Na haiwapi Israel ulinzi wa kusogea mbele, kama wanavyotaka Waisrael," amesema Mladenov.

“Tunausitishaji wa mapigano. Unafanya kazi. Haujakamilika. Kuna ukiukwaji kila siku, na baadhi ni ukiukwaji mkubwa," amesema, akimaanisha ukiukwaji unaoendelea kufanywa na Israel.

Jitihada za Trump za amani

Bodi ya Amani imeundwa Januari kwa jitihada za Rais wa Marekani Donald Trump kama sehemu ya kufikia makubaliano ya amani Gaza.

Marekani baadae ilisema nchi nyengine zilijiunga katika jitihada hiyo.

Tangu kusitishwa kwa mapigano Oktoba 10, 2025, mashambulizi ya Israel yameuwa takriban Wapalestina 856 na kujeruhi 2,463, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifanyika baada ya miaka miwili ya mauaji ya halaiki Gaza yaliyoanza Oktoba 2023.

Mashambulizi ya Israel baadae yaliendelea katika mfumo tofauti, na kuuwa zaidi ya Wapalestina 72,000, kuwajeruhi zaidi ya 172,000 na kuharibu takriban asilimia 90 ya miundombinu ya raia Gaza.