Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametoa ujumbe siku ya Jumapili akiadhimisha miaka 104 ya Siku ya Ushindi, ikiwa ni kumbukizi ya ushindi mkubwa katika Vita vya Uhuru wa nchi.
"Leo, tuna fahari ya kuadhimisha miaka 104 ya Ushindi Mkubwa, ambao umeingia katika historia kama 'Mapigano ya Amiri Jeshi Mkuu' na kuwa hatua muhimu kabisa katika Mapambano ya Taifa," Erdogan amesema katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano kupitia mtandao wa kijamii wa Uturuki NSosyal.
"Nalipongeza taifa letu pendwa, Waturuki wa Kupro na raia wetu wanaoishi katika nchi mbalimbali duniani katika Siku ya Ushindi ya Agosti 30.
"Nawapongeza kwa dhati wageni wetu ambao wanafurahi na sisi katika siku ya mapumziko katika balozi zetu nje."
Erdogan amesema ushindi wa Agosti 30 kwa mara nyengine unathibitisha kwamba ardhi ambayo taifa la Uturuki limekuwepo kwa uhuru kwa maelfu ya miaka ni "makazi yake ya kudumu."
"Ushindi Mkubwa, ambao pia umefungua milango ya kuundwa kwa Jamhuri, ulitangaza kwa dunia nzima kwamba taifa letu kamwe haliwezi kukubali kukaliwa, huku pia ikisaidia kuvunja mzingiro wa kibeberu katika eneo letu," amesema.
"Ari, na azma tuliyoonesha kama taifa miaka 104 iliyopita licha ya kuwepo kwa changamoto inabaki kuwa chanzo cha ari yetu leo."
Historia iliyotukuka
Erdogan amesema Uturuki, ikihimizwa na "historia yake iliyotukuka," inaendelea kutimiza malengo yake kupitia simulizi za mafanikio katika kila nyanja, kuanzia nishati na ulinzi mpaka sayansi, teknolojia, na sera ya mambo ya nje.
"Katika nyakati ambazo, vita, migogoro, na hali ya kisiasa isiyotabirika ikiongezeka duniani, hasa katika kanda yetu, Uturuki inasimamia sera zake ambazo zimejikita katika misingi ya haki za binadamu," amesema.
"Napenda kusema kwamba leo hii kuna Uturuki ambayo inapambana kuzuia unyanyasaji bila kujali nani anayeufanya, inasimama na wanaodhulumiwa bila kujali ni kina nani, na haisiti kuchukua hatua inapolazimika kwa ajili ya hilo."
Akinukuu msemo wa Kituruki wa kale, Erdogan amesema: "Labda mbingu za buluu zianguke na ardhi kupasuka, hakuna atakayeweza kuifanya Uturuki na taifa la Uturuki kuacha mapambano yake yaliyobarikiwa."
"Licha ya uchokozi unaofanywa na wanaonufaika na vurugu, sisi, kama taifa, tutaendelea kusimamia haki, sheria, amani na utulivu," amesema.
Karne ya Uturuki
Erdogan amewashukuru raia wote walio, "kama miaka 104 iliyopita," wamechangia katika umoja na mshikamano kujenga Karne ya Uturuki.
"Katika siku hii muhimu, pia naungana kwa upendo na marafiki zetu wote wanawake na wanaume katika kila pembe ya dunia ambao mioyo yao iko pamoja nasi katika furaha na huzuni," amesema.
"Katika siku hii, naadhimisha kwa shukran Gazi Mustafa Kemal Ataturk, amiri jeshi mkuu wa Ushindi Mkubwa, na wenzake katika jeshi. Namuomba Mwenyezi Mungu rehema zake ziwe kwa mashahidi wetu, ambao tunawaona kama waongozi wa uhuru wetu, na kuwakumbuka mashujaa wetu kwa kuwashukuru.
"Siku ya Ushindi, yenye furaha ya Agosti 30."
Siku ya Ushindi inaashiria mwisho wa vita magharibi mwa Anatolia dhidi ya vikosi vya Ugiriki mwaka 1922 na ni kwa ajili ya Vikosi vya Ulinzi vya Uturuki.
Vikosi vya Uturuki vilipambana katika Vita vya Dumlupinar kuanzia Agosti 26 sehemu ambayo leo inajulikana nchini Uturuki kama mkoa wa kati ya Kutahya, ambapo vikosi vya Ugiriki vilivyovamia vilisambaratishwa.
Kufikia mwishoni mwa 1922, vikosi vyote wa kigeni vilitimuliwa katika maeneo ambayo mwishowe kwa pamoja yalikuwa Jamhuri ya Uturuki mwaka mmoja baadae.





















