James Kidega kutoka Tanzania, miongoni mwa walimu bora duniani
James Kidega David, mwalimu wa shule ya sekondari ya Kiara nchini Tanzania, ameorodheshwa miongoni mwa walimu 50 bora katika Tuzo ya Mwalimu Bora Duniani
Mtanzania James Kidiga David ambaye ni mwalimu wa lugha ya Kiingereza na jiografia katika Shule ya Sekondari ya Kiara, ametajwa katika walimu 50 bora duniani kwenye tuzo ya Mwalimu Bora Duniani 2023.
Tuzo hiyo ya Mwalimu Bora Duniani, hukabidhiwa kwa walimu ambao hujitolea katika njia mbalimbali kuanzia kufundisha mijini na vijijini, kutetea ujumuishaji na haki za watoto, kuunganisha wahamiaji katika madarasa na kukuza uwezo na ujasiri wa wanafunzi wao.
Shule ya Sekondari ya Kiara ina wanafunzi 900 kwa jumla, na darasa la James likijumuisha kati ya wanafunzi 55 hadi 60 wenye umri wa miaka 13-16. Wanafunzi na walimu katika shule hiyo wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo msongamano wa wanafunzi madarasani, ukosefu wa mahitaji ya shule na ukosefu wa taulo za kike kwa wasichana.
James, ambae ni mwalimu pekee katika shule yake anayetumia teknolojia darasani, amewekwa kwenye orodha ya mwalimu bora duniani kwa kuanzisha shirika lake binafsi, liitwalo Pamoja Hub, ambalo, lilizindua kampeni ya kutoa usafi kwa wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kiara na Shule ya Sekondari ya Nyasho.
Aidha, kwa kupitia Shirika lake la Pamoja Hub, James pia amefanikiwa kuwaepusha vijana wapatao 2300 dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na changamoto za hedhi kupitia kampeni zake kuu ambazo alizoziita 'ShuleKwanzaTz' na 'Siku Salama, Mafunzo Salama'.
Kwa sasa James yuko katika utekelezaji wa mradi ' PamojaDigitalks '(mazungumzo juu ya teknolojia).
Wakati huo, alipata fedha kupitia Shirika la World Literacy Foundation na hivyo basi kuwawezesha vijana 80 kupata sare za shule na vitabu, mbali na kuongoza kampeni ya kukomesha tamaduni hatari ya ndoa za mapema na ukeketaji wa wanawake katika jamii yani FGM.
James hujitolea kama mratibu wa kikanda katika Chama cha Walimu wa lugha ya Kiingereza Tanzania (TELTA) huko Mara, na ndani ya miaka miwili tu, amefikia na kuimarisha zaidi ya walimu wa lugha ya Kiingereza 500 katika wilaya tano katika mkoa wa Mara.
Walimu hao wanatoka katika maeneo mbalimbali ikiwemo Rorya vijijini, Bunda vijijini, Bunda mjini, Musoma mjini na vijijini ambapo walibadilishana mawazo juu ya mbinu za ujuzi na mbinu za kisasa za kufundisha na kuunganisha teknolojia katika madarasa.
Tuzo hii pia, inakuja wakati walimu duniani wanaadhimisha siku yao maarufu Siku ya Walimu Duniani, ambapo mbali na mafanikio na machango wao mkubwa katika jamii, lakini bado baadhi hasa wanaotoka mataifa yanayoendelea, wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo malipo duni pamoja na ukosefu wa zama bora za kufundishia.