| Swahili
AFRIKA
3 DK KUSOMA
Waziri Mkuu Tanzania apiga ‘Stop’ makampuni binafsi upimaji ardhi
Waziri Mkuu nchini Tanzania Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.
Waziri Mkuu Tanzania apiga ‘Stop’ makampuni binafsi upimaji ardhi
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaaliwa. Picha PMO / Others
6 Oktoba 2023

Waziri Mkuu nchini Tanzania Kassim Majaliwa ameagiza kampuni zote zilizopewa kazi za upimaji wa viwanja kwenye Jiji la Dodoma na zimeshindwa kukamilisha kazi hiyo, ziwe zilikuwa na mikataba ama hazikuwa na mikataba zichukuliwe hatua kali za kisheria.

“Moja kati ya hatua hizo, ni kuziblacklist kwa sababu makampuni hayo yapo, tutumie makampuni ambayo yana uaminifu badala ya kutumia makampuni ambayo yanatuzalishia migogoro,” ameagiza Waziri Mkuu Majaaliwa.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo na kutafuta suluhisho.

“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao.”

Wakati huo huo, Majaaliwa aliwaagiza Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa Kamishna Msaidizi wa Mkoa, Maafisa Mipango Miji wa Majiji, Halmashauri na Manispaa hawana sababu ya kuchukua watumishi wa muda kufanya kazi ya upimaji bali wafanye wao ili kuepusha mianya ya rushwa.

“Tunatambua makampuni mengi hapa Dodoma ni ya watumishi wenyewe kama ambavyo imeelezwa kwenye ripoti. Mkurugenzi alikuwa na kampuni mbili, Mhasibu wake ana kampuni yake na wanazitumia kupima maeneo, kwa hiyo ni miradi yao.”

- Kassim Majaaliwa, waziri mkuu wa Tanzania

Agizo hili linakuja wakati ambalo, kumekuwa na ongezeko la migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali ya nchi. Tafiti zinaonyesha baadhi ya migogoro hiyo husababishwa na baadhi ya makampuni yaliyopewa jukumu la kupima viwanja na hatimae kuviuza.

Tangu serikali kuhamia rasmi jijini Dodoma, kumekuwa na mahitaji makubwa ya manunuzi ya viwanja kutokana zaidi ya watumishi wa umma laki moja na nusu kuhamia jijini humo.

Ikumbukwe pia, katika kipindi cha miaka miwili, tayari rais wa Tanzania Samia Sulumu Hassan ashafanya mabadiliko ya uongozi wa Wizara ya Ardhi mara mbili, hii ikionekana moja wapo ya hatua za kuboresha utendaji wa wizara hiyo ambayo inakabiliwa na migogoro mingi ya ardhi.

CHANZO:TRT Afrika