Uturuki inamkumbuka Ataturk miaka 87 baada ya kufariki

Rais wa Uturuki, viongozi wa vyama vya siasa, maafisa waandamizi wa mahakama, maafisa wa jeshi, watumishi wengine wa serikali walikusanyika Anitkabir jijini Ankara kumkumbuka Mustafa Kemal Ataturk, muasisi na rais wa kwanza wa nchi.

By
Erdogan aliweka mashada ya maua mekundu na meupe yenye muundo wa bendera ya Uturuki katika kaburi la Ataturk.

Mustafa Kemal Ataturk, muasisi wa Jamhuri ya Uturuki, alikumbukwa siku ya Jumatatu miaka 87 tangu alipofariki kwa hafla rasmi ya kitaifa Anitkabir, makumbusho alipozikwa katika mji mkuu Ankara.

Hafla hiyo ilianza kwa kushiriki kwa Rais Recep Tayyip Erdogan, Spika wa Bunge Numan Kurtulmus, mawaziri, viongozi wa vyama vya kisiasa, maafisa waandamizi wa mahakama, na makamanda wa kijeshi.

Erdogan aliweka mashada ya maua mekundu na meupe yaliyowekwa kwa muundo wa bendera ya Uturuki katika kaburi la Ataturk.

Saa tatu na dakika tano asubuhi, muda hasa aliofariki Ataturk, walioshiriki walikaa kimya kwa muda, na baadaye kuimbwa wimbo wa taifa. Wakati wa kutoa heshima, bendera ya Uturuki ilishushwa nusu mlingoti.

Baadaye, Erdogan na maafisa aliyoandamana nao walielekea katika eneo la Misak-i Milli, ambapo alitia saini Kitabu cha Kumbukumbu cha Anitkabir, akitoa heshima zake kwa Ataturk na wenzake waliopigania taifa.

"Kwa dhati kabisa tunalinda Jamhuri ya Uturuki, ambayo uliiita kuwa 'kazi kubwa,' na kuendelea kupamba kila sehemu ya nchi yetu na mafanikio mapya," Erdogan aliandika.

"Chini ya uongozi thabiti na viongozi waliobobea, Uturuki inaimarika na kwa ujasiri ili kuwa nchi yenye uwezo duniani," aliongeza.

Ataturk alikuwa rais wa kwanza wa jamhuri hadi Novemba 10, 1938, alipofariki jijini Istanbul akiwa na umri wa miaka 57 kutokana na maradhi ya ini.

Kwa kawaida watu wa Uturuki hutembelea kaburi lake kila Novemba 10 kutoa heshima zao kwa muasisi wa taifa.