Zulfa, bondia wa kike Tanzania anayetesa anga za kimataifa
Zulfa, ana historia kubwa nchini Tanzania, alichagua mchezo wa ngumi kuwa kazi kama ilivyo kazi nyingine na imeweza kumpatia ajira katika jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Suleiman Jongo
TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania
Endapo utapata fursa ya kutembelea Gym inayojulikana ‘Uwanja wa Kivita‘ iliyopo jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania, basi utakutana na mabondia kadhaa wa kike akiwemo Zulfa Macho wanaofanya mazoezi na kupigana mapambano mbalimbali ya kimataifa.
Zulfa, ana historia kubwa nchini Tanzania, aliyechagua mchezo wa ngumi kuwa kazi kama ilivyo kazi nyingine na imeweza kumpatia ajira katika jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) sababu ya ndondi.
Na katika kuonyesha kuwa mchezo huu sio wa wanaume pekee, basi mara nyingi mabondia wa kike wanafanya mazoezi ya kupigana na mabondia wanaume. Na Zulfa, anayepigana katika uzito wa Superfly ni miongoni mwao.
Waswahili husema maji siku zote hufuata mkondo na mtoto wa nyoka siku zote ni nyoka.
Zulfa anatoka kwa familia ya michezo
Tofauti tu ni kwamba, baba yake mzazi, Yusuf Macho, alikuwa ni mchezaji wa timu ya taifa soka ya Tanzania, Taifa Stars na kuchezea vilabu kadhaa ikiwemo Simba Sports Club na yeye ( Zulfa) ni bondia.
Kwa Zulfa, kwake yeye, kila mtu siku zote anacho anachokipenda. Na masumbwi, au vitasa kama vinavyojulikana kwa sasa nchini Tanzania ndio chaguo lake.
TRT Afrika, wakati inafanya mahojiano na Zulfa, ilitaka kujua, kwa nini hakuchagua michezo mingine, ukiwemo mchezo wa soka au kandanda aliocheza baba yake kwa mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa au mpira wa Pete ( Netball) au riadha?
Zulfa, ambaye ikiwa utapenda kumuita ‘Malkia wa masumbi‘ utakuwa hujakosea, anasema ushabiki wa ngumi alikuwa nao toka akiwa mdogo, akipendelea pia kuangalia mapambano makubwa na maarufu duniani yakiwemo yale ya Mike Tyson.
Lakini, siku zote , ili uweze kupata mafanikio, basi jitihada zinahitajika. Na Waswahili husema, siku zote hakuna kazi rahisi.
Katika kutimiza ndoto zake za kuwa bondia mwenye mafanikio, Zulfa alipita katika milima na mabonde, ili kupata anachokihitaji. Anasema ukitaka kuvua samaki, ni vizuri ukajua pia kuogelea. Hivyo, naye alikubali vipigo katika mazoezi ili awe bondia mzuri.
Alipoulizwa, anajisikiaje pale anapopigwa ulingoni, Zulfa anakiri kwamba hakuna bondia anayependa kupigwa ulingoni, lakini kwa kuwa ni sehemu ya mchezo, imekuwa ni kawaida.
“Kupigwa katika ngumi ni sehemu ya mchezo, kama ilivyo katika mpira wa miguu, ushindi, sare au kupoteza ni sehemu ya matokeo na ndio raha ya mchezo wenyewe kwa mashabiki,“anasema Zulfa.
Lakini wakati mwingine, huzuni hutawala katika kambi ya bondia au familia yake pale anaporejea nyumbani akiwa amevimba uso kutokana na kipigo.
"Familia inabidi izoee hali hii,“
“Kama atakuwa mume, basi itabidi amfariji bondia mkewe baada ya pambano,”
“Na kama bondia aliyepigwa atakuwa ni mwanaume, basi mke pia itabidi amfariji mume wake baada ya pambano, ikiwemo kuendelea kumpa huduma nyumbani ya kumkanda sehemu aliyoumia,”
"Baada ya kupewa huduma ya kwanza ulingoni, basi inabidi huduma ya kwanza nyingine iendelee pia nyumbani baada ya kutoka ulingoni,” anasema Zulfa.
Na katika mapambano mengi aliyocheza Zulfa, ikitokea ameshindwa pambano, basi furaha na amani bado vitaendelea kutawala katika kambi yake au familia yale kwa sababu yeye amechagua mchezo wa ngumi na hii ni sehemu ya maisha yake kwa sasa.
“Kushindwa ni sehemu ya mchezo na kunakufanya uweze kujiuliza na kujipanga vizuri kwa ajili ya pambano lingine.”
“Ndio maana kocha anafanya tathmini baada ya pambano ili kujua wapi nilikosea na kusonga mbele,”anasema Zulfa mwenye miaka 23.
Lakini kwa bahati nzuri, katika mapambano yake matano ya ngumi za kulipwa aliyocheza, Zulfa ameshinda yote. Alifanikiwa kumpiga Halima Vunjabei (Tanzania), aliyempiga mara mbili, Ndau Chilimba kutoka Malawi, Flora Machela ( Tanzania) na Alice Mbewe (Zambia).
Katika moja ya mapambano hayo, alimpiga Halima katika pambano la ngumi la kulipwa la uzito wa kilo 52 na kutwaa ubingwa wa Dunia (UBO) Uzito wa Superfly wa kumsaka Malkia wa masumbwi nchini mwaka 2021.
Lakini mwaka mmoja kabla (2020), Zulfa alionyesha cheche katika ulingo wa kimataifa baada ya kumshinda bondia Alice Mbwewe wa Zambia.
Pambano hili lilikuwa moja ya mapambano ya utangulizi katika pambano la Superwelt kati ya Mtanzania Hassan Mwakinyo na Jose Carlos Paz wa Argentina.
Mafanikio haya yote yaliweza kumfanya Zulfa kutengeneza vichwa vya habari kitaifa na kimataifa.
Katika moja ya michezo ya hivi karibuni ( 2023), Zulfa alianza vizuri mashindano ya kufuzu Olimpiki ya Paris mwaka 2024 kwa Bara la Afrika, baada ya ushindi wa points 5-0 dhidi ya Grace Nankinga wa Uganda katika uzito wa Fly katika pambano lililofanyika Dakar, Senegal.
Kwa ushindi huo, Zulfa ameingia hatua ya 16 Bora na atapambana na Adeiola Oyesiji wa Nigeria.
“Mimi siku zote najiamini katika mapambano yangu na nashukuru kocha wangu ananipa mazoezi ya kutosha,” anasema Zulfa.
“Mapambano niliyopambana ni mengi kwa kweli, lakini nashukuru Mungu kwa mafanikio ninayoyapata hasa katika ngumi za kimataifa. Kupitia ngumi, napata kipato cha kuendesha maisha yangu. Ndio mchezo niliouchagua, umenipa kazi na unanipa maisha na kuonyesha nguvu ya mwanamke ulingoni,“ anasema Zulfa.
Zulfa anasema mchezo wa ngumi ni mchezo hatari, ambapo mtu anaweza kuumia na hata kufa, hivyo unahitaji uvumilivu wa hali ya juu.
Mmoja wa mabondia wanawake wanaofanya mazoezi pamoja na Zulfa, Nasra Msami anamzungumzia Zulfa kama bondia mzuri na mwenye mazoezi.
“Hana mechi nyingi kimataifa, lakini zile chache alizocheza amefanya vizuri na kuiwalikisha vema Tanzania,“ anasema Msami.
“Ana bidii ya mazoezi na kujituma ulingoni“ “Lakini pia ni mvumilivu na hakati tamaa na hii itamfikisha mbali,“ anasema Nasra.
Msami na Zulfa, pamoja na mabondia wengine wa kike na kiume wanafanya mazoezi pamoja katika Gym yao.
Kocha Mkuu wa Gym hiyo, Kwame Said anasema Zulfa ni miongoni mwa mabondia wake anaowakubali sana.
“Ana bidii kubwa sana mazoezini na anasikiliza kila ninachomuelekeza. Namuona kama bondia mwenye mafanikio makubwa sana katika siku za usoni,“ anasema kocha Kwame.