Rais Trump atishia kuharibu boti yoyote itakayokaribia eneo la kizuizi kilichowekwa na Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa onyo kali dhidi ya boti zozote za Iran za mashambulizi zitakazokaribia eneo la kizuizi cha baharini kilichowekwa na Marekani karibu na bandari za Iran.
Rais Trump pia alisema jeshi la Marekani litatumia “mfumo uleule wa kuua” uliotumika dhidi ya boti za wauza dawa za kulevya baharini, akiashiria mashambulizi ya anga dhidi ya boti zinazodaiwa kubeba mihadarati karibu na pwani ya Venezuela.
Haya yanajiri baada ya zuio la Marekani dhidi ya kila aina ya usafiri wa baharini unaoingia na kutoka katika bandari za Iran kuanza kutekelezwa.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imeanza kutekeleza zuio dhidi ya kila aina ya usafiri wa baharini unaoingia na kutoka katika bandari za Iran, ikilenga meli zilizoko katika Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman.
CENTCOM imesema kuwa hatua hizi zitatekelezwa “kwa usawa dhidi ya meli za mataifa yote,” hata hivyo imesisitiza kwamba usafiri kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz kuelekea na kutoka bandari zisizo za Iran hautaathirika.