Na mwandishi wetu
TRT Afrika, Dodoma, Tanzania
Baada ya shutuma nzito kuelekzwa kwa Jeshi la Polisi nchini Tanzania likidaiwa kuwatesa baadhi ya raia katika maeneo mbalimbali nchini humo, Jeshi hilo limejitokeza hadharani na kudai kuanzisha rasmi uchunguzi wa malalamiko hayo.
Kulingana na taarifa iliyotumwa katika mitandao ya kijamii ya Jeshi hilo na ambayo TRT Afrika ilipata nakala yake, msemaji wa Jeshi hilo nchini Tanzania David Misime amekiri kuona taarifa ya tuhuma hizo dhidi ya Jeshi la Polisi na kuahidi uchunguzi kuanza rasmi.
Kauli hii inakuja siku moja baada ya kusambaa kwa taarifa katika vyombo mbalimbali vya habari za kudai kunyanyaswa kwa baadhi ya raia akiwemo Kalamba Mnenge, mkazi wa Dodoma. Mnenge anaedai kukamatwa na hatimae kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Nkuhungu mjini Dodoma, kuteswa na kudhalilishwa. Mnenge, mwenye umri wa miaka 38 na ambae ni mfugaji, alielezea baadhi ya masaibu aliyopitia.
“Walinifunga pingu miguuni na mikononi na kisha kunitupia kwenye gari lao. Wakati wote sikujua ni wapi naeleka, lakini kuna sehemu walisimama na kupakia magunia ya mkaa na nilipochungulia niligundua wamenipeleka kituo cha polisi cha Nkuhungu,” anasema.
Taarifa ya Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake David Misime ilisema ili kuhakikisha haki inatendeka, Jeshi hilo litashirikisha wataalamu wengine wa haki jinai ili kufanikisha uchunguzi wa malalamiko hayo na pia kutoa fursa kwa wananchi wenye ushahidi wowote kujitokeza na kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukamilisha uchunguzi huo mapema.
Kwa upande wake, Mnenge ameomba kupewa msaada wa kisheria utakayomsaidia kupata haki zake za msingi baada ya kudai pia kunyanyaswa kijinsia.
“Matumani yangu ni kupata msaada wa kisheria kwa sababu mbali ya kupoteza mali zangu ikiwemo mifugo, lakini pia nimenyanyaswa kijinsia," anasema.
Wakati hayo yakijiri, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno, ameitisha mkutano wa hadhara ambapo anataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kutoa kero zao.
Hatua hii inakuja siku moja tu, baada ya kusema Jeshi la Polisi halikuwa na taarifa ya kukamatwa kwa kijana huyo ingawa aliahidi kulifanyia uchunguzi.
“Sisi kama Jeshi la Polisi kuna hatua tunazochukua. Kwanza tukishapokea malalamiko ya mlalamikaji tutachunguza na tukibaini kuna mtendaji wetu amekwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Polisi hatua za kisheria zitachukuliwa na wakati mwingine tukibaini tunakwenda mbali zaidi kwa kumfukuza kazi na kumfikisha Mahakamani,” amesema Otieno.












