Felix Tshisekedi akaribia kushinda uchaguzi wa urais DRC

Matokeo yote ya awali yaliyotolewa kufikia sasa baada ya uchaguzi mkuu wa Disemba 20, yanaonyesha Rais Felix Tshisekedi akiongoza ingawa wapinzani wamepuuza matokeo hayo.

By Nuri Aden
Rais wa sasa wa DRC Félix Tshisekedi / Picha: AFP / AFP

Rais wa sasa wa DRC Félix Tshisekedi anaonekana kushinda uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliofanyika tarehe 20 Disemba huku akiongoza kwa kupokea zaidi ya asilimia 70 ya kura tangu matokeo ya awali ya Alhamisi jioni.

Kufikia sasa, Tshisekedi amepata milioni 9.5 kati ya kura milioni 12.5 zilizohesabiwa na kuacha mwanya mkubwa kati yake na washindani wake wa karibu.

Hata hivyo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) bado haijakamilisha kutangaza matokeo yote huku mshindi wa uchaguzi wa urais DRC, akitarajiwa kutangazwa rasmi tarehe 10 Januari 2024, na Mahakama ya kikatiba.

Hata hivyo, serikali ya DRC imepiga marufuku marudio ya uchaguzi licha ya baadhi ya waangalizi kueleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya dosari za uchaguzi.

Ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya SADC ,DRC maarufu SEOM 2023, unaongozwa na aliyekuwa makamu wa rais wa Zambia Enock P. Kavindele yenye waangalizi 72 kutoka mataifa sita (6) wanachama wa SADC: Angola, Namibia, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe na Tanzania, imetoa wito kwa pande zote za kisiasa DRC kudumisha amani.

Ujumbe wa uchaguzi kutoka SADC, unawapongeza raia wa DRC kwa kuendelesha uchaguzi kwa njia ya amani na utulivu wakati wa kupiga kura.

Mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa gavana wa Katanga Moïse Katumbi ndiye anamfuata Tshisekedi akiwa na asilimia (16.5%) ya kura huku mpinzani mwingine, Martin Fayulu akiwa na asilimia (4.4%).