Afrika Kusini kubatilisha viza 2,000 zilizopatikana kwa njia isiyo sahihi baaada ya uchunguzi

Ripoti imeonesha mfumo wa uhamiaji wa Afrika Kusini umetumiwa vibaya kwa miaka na kundi la maafisa wachache ambao wamejitajirisha kwa kupokea malipo kwa kutoa viza.

By
SIU ilisema imefanya rufaa za kesi za jinai 275 kwa Mamlaka ya Kuchunguza Kesi za Kitaifa. / Others

Afrika Kusini inajiandaa kufuta zaidi ya viza 2,000 ambazo zimepatika kwa njia isiyo sahihi, huku serikali ikiendesha msako mkali wa rushwa ndani ya Idara ya Mambo ya Ndani.

Waziri wa Mambo ya Ndani Leon Schreiber amesema mamlaka vinapitia mchakato wa kiutawala kubatilisha viza ambazo zinaaminika kutolewa kupitia mitandao ya rushwa baada ya mfumo wa uhamiaji kuchezewa.

“Tunaangalia mchakato wa kiutawala ili tufute zaidi ya viza 2,000 ambazo zimetolewa kwa njia ambayo sio sahihi," amesema Schreiber.

Hatua hiyo inafuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na Kitengo Maalum cha Uchunguzi (SIU), ambacho kimeibua nyaraka zilizoghushiwa, utoaji na upitishaji wa viza usio wa kawaida, na mtandao wa uwezeshaji unaoruhusu watu kuingia Afrika Kusini kinyume cha sheria.

Matokeo ya uchunguzi

Schreiber amewaambia waandishi wa habari mjini Pretoria kwamba hatua za kinidhamu tayari zimechukuliwa dhidi ya maafisa waliopatikana na hatia.

“Pia tuna rufaa za uhalifu 275 kupitia kazi hii, na kesi za uchunguzi 111 ambazo zimefungwa,” amesema Schreiber.

Tangu Aprili mwaka jana, maafisa 20 wa Mambo ya Ndani wamefutwa kazi na wengine 16 kusimamishwa kwa muda.

Mfumo wa Afrika Kusini wa uhamiaji umetumiwa vibaya kwa miaka mingi na kundi ndogo la maafisa ambao wamejitajirisha kwa kupokea malipo kwa kutoa viza, na vibali vya kuishi, kwa mujibu wa uchunguzi wa serikali.

Rais Cyril Ramaphosa, alitoa amri ya kufanyika kwa uchunguzi unaohusisha kutolewa kwa viza kati ya mwaka 2004 mpaka 2024, kabla ya kuunda kwa serikali ya pamoja.

Mbali na hatua hizo binafsi, serikali pia imesema inafanya udhibiti katika idara ya uhamiaji na kuziba mapengo yenye kuleta rushwa.

Mapato kutokana na rushwa

Maafisa walioachishwa kazi hawakutajwa kwa majina, lakini uchunguzi unaonesha wanne kati yao walipokea zaidi ya randi milioni 16 (dola za Marekani milioni 1), ilisema taarifa ya Kitengo Maalum cha Uchunguzi (SIU).

Mmoja aliijenga jumba, wakati wengine walinunua mali kwa fedha taslimu, ilisema taarifa hiyo.

“Matokeo haya yanaonyesha kwamba rushwa katika mfumo wa viza ni ya kupanga, na kudhamiria, na inapoteza imani ya umma,” SIU ilisema.

Ilisema kwamba imegundua "hali yenye kusababisha hofu: mfumo wa uhamiaji wa Afrika Kusini umeonekana kama soko, ambapo vibali na visa vilikuwa vinauzwa kwa mpigaji wa juu zaidi."

Maombi kwa kawaida yalitumwa kupitia WhatsApp kwa ajili ya idhini ya haraka, kisha malipo yalifanywa kwa wake wa maafisa hao, ilisema. Katika matukio mengine, pesa taslimu zilifichwa ndani ya fomu za maombi.

Waziri wa Mambo ya Ndani Leon Schreiber alisema idara yake inafanya kazi kukomesha udanganyifu hasa kwa kubadilisha mifumo yake kuwa ya kielektroniki.

“Ni kupitia mageuzi ya mfumo yanayozingatia mabadiliko ya kidigitali na matumizi ya teknolojia za kisasa tu ndipo tunaweza kuzuia kabisa rushwa,” alisema.

SIU ilisema imefanya rufaa za kesi za jinai 275 kwa Mamlaka ya Kuchunguza Kesi za Kitaifa. Schreiber alisema maafisa 20 wa Idara ya Mambo ya Ndani wameachishwa kazi tangu Aprili mwaka jana.