Morocco imewafunga Uholanzi kupitia mikwaju ya penati na kufuzu hatua ya timu 16 katika Kombe la Dunia siku ya Jumatatu baada ya awali kumaliza kwa matokeo ya 1-1 huko Monterrey.
Golikipa wa Morocco Yassine Bounou aliokoa mkwaju wa tano wa Uholanzi uliopigwa na Crysencio Summerville na mshambulizi Ismael Saibari akaingia na kufunga penati ya ushindi iliyofanya matokeo kuwa 3-2.
Ushindi huo umevusha Morocco hadi hatua ya timu 16 na itaikabili Canada huko Houston, Marekani siku ya Jumamosi.
Mechi hiyo iliyokuwa na msisimko mkubwa iliendelea hadi muda wa ziada baada ya Issa Diop kufunga goli la kusawazisha la Morocco katika muda wa nyongeza wakati Uholanzi ikikodolea macho ushindi.
Uholanzi ilikuwa imefunga goli kipindi cha pili kupitia mshambuliaji wa Liverpool Cody Gakpo, akiwa anacheza siku chache baada ya mwenza wake kuthibitisha kifo cha mtoto wao wa kiume akiwa tumboni.
Mchezaji huyo wa Liverpool Gakpo alionekana kuwa na hisia kali huku wenzake wakimkumbatia kwa muda mrefu kama kumfariji.
Lakini Morocco ikasawazisha katika muda wa ziada wakati Diop alipopiga kichwa kutokana na ‘cross’ ya Chemsdine Talbi.
Morocco ilikuwa na nafasi nyingi zaidi, katika mechi iliyokuwa na vuta ni kuvute nyingi, wachezaji wakimtafuta ubaya mwamuzi kutoka Brazil Wilton Sampaio.
















