Armenia: Helikopta ya Waziri Mkuu yatua kwa dharura kufuatia hali mbaya ya hewa
Waziri Mkuu Nikol Pashinyan amesema kuwa tukio hilo limetokea karibu na eneo la Vanadzor, ambalo ni la tatu kwa ukubwa nchini Armenia.
Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan amesema siku ya Jumamosi kuwa helikopta yake ilitua kwa dharura kutokana na uwepo wa hali mbaya ya hewa.
Tukio hilo limetokea karibu na Vanadzor, mji wa tatu kwa ukubwa nchini humo na mji mkuu wa jimbo la Lori, aliandika Pashinyan kwenye ukurasa wake wa Facebook.
"Imebidi helikopta yetu itue kwa dharura katika eneo la Vanadzor kutokana na hali mbaya ya hewa.
Kwa sasa, tunaendelea na safari yetu kwa gari. Nawatika siku njema," alisema.
Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, waziri mkuu alikuwa akielekea kwenye makazi ya Baganis kwenye mpaka na Azerbaijan, ambapo mpaka huo uliwekwa hivi karibuni.