Afrika Mashariki yawasilisha bajeti ya dola milioni 112

Jumuiya hiyo yenye nchi wanachama nane, imeweka malengo hayo baada ya kuwasilisha bajeti ya dola milioni 112 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

By Edward Josaphat Qorro
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki, Deng Alor Kuol akijiandaa kuwasilisha bajeti ya Jumuiya hiyo kwa mwaka wa fedha 2024.2025./Picha: EALA X / Others

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeazimia kuimarisha amani ya kikanda baada ya kuwasilisha bajeti ya dola milioni 112, Juni 25, 2024, jijini Arusha nchini Tanzania.

Jumuiya hiyo, yenye nchi wanachama 8, pia imelenga kuimarisha uwekezaji na biashara ya kikanda kupitia bajeti hiyo, wakati wa mkutano wa 4 wa kikao cha pili cha bunge la tano la EALA.

Mara baada ya wasilisho la bajeti hiyo na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Afrika Mashariki kutoka Sudan Kusini Deng Alor Kuol, wabunge 63, kutoka nchi wanachama watapata siku mbili za kuisoma na kuijadili bajeti hiyo.

Bajeti hiyo, pia itaangazia uanzishwaji wa taasisi za fedha kuelekea mchakato muhimu wa kuwa na sarafu ya pamoja.

Kulingana na Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki, dola milioni 67.7 ni vyanzo vya ndani kutoka nchi wanachama wakati dola milioni 43.9, inahusisha michango kutoka washirika wa maendeleo.

Katika mwaka wa fedha uliopita, EALA ilipitisha bajeti ya dola milioni 103.8, katika kufanikisha shughuli mbalimbali za Jumuiya hiyo, yenye makao yake makuu jijini Arusha nchini Tanzania.

Hata hivyo, pamoja na kuwasilisha bajeti hiyo, baadhi ya wajumbe wameonesha wasiwasi wao juu ya mwenendo wa michango kutoka nchi wanachama na hivyo kuathiri baadhi ya shughuli za mihimili ya Jumuiya hiyo, ikiwemo EALA yenyewe na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ).

"Wakati Tanzania, Kenya na Uganda zinawasilisha michango yao asilimia 100, bado nchi zingine zinasuasua kufikia malengo hayo," amesema James Millya, mjumbe kutoka Tanzania.

Mwenendo usioridhisha wa nchi wananchama kuwasilisha michango yao kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa sasa.

Baadhi ya wabunge wa EALA, wanaharakati na watu kutoka kada mbalimbali wametaka nchi zinazishindwa kutimiza sharti hilo la kisheria, kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo.

Pata habari zaidi kupitia whatsapp channels