Mtanzania Faustine Ndugulile achaguliwa kuwa bosi wa WHO Afrika

Dkt Faustine Ndugulile alipata kura 25, dhidi ya jumla ya kura 20 kutoka kwa wapinzani wake wawili kutoka nchi za Senegal na Niger, katika uchaguzi uliofanyika mjini Brazzaville, Jamhuri ya Congo.

By Edward Josaphat Qorro
Dkt Faustine Ndugulile.Picha:TRT Afrika / Others

Mtanzania Faustine Ndugulile ndiye Mkurugenzi mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kanda ya Afrika.

Dkt Ndugulile, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam na aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia nchini Tanzania, anachukua nafasi hiyo baada ya kuwashinda wapinzani wake wa karibu kutoka Senegal na Niger, wakati wa mkutano wa 74 wa WHO kwa kanda ya Afrika, unaofanyika kati ya Agosti 26 hadi 30, mjini Brazzaville katika Jamhuri ya Congo.

Dkt Ndugulile aliwashinda Dkt Ibrahima Socé Fall kutoka na Senegal na Dkt Boureima Hama Sambo wa Niger, yeye akiwa amekusanya kura 25, dhidi ya 20 za wawili hao.

Naibu huyo wa Afya wa zamani nchini Tanzania, sasa anachukua nafasi ya Mbotswana Matshidiso Moeti, alihudumu katika nafasi hiyo ya uongozi kutoka mwaka 2015, na kuwa mwanamke wa kwanza kushukilia nafasi hiyo barani Afrika.

Dkt Ndugulile anatarajiwa kuanza rasmi kazi mwezi Februari 2025, ambapo anategemewa kuhudumu nafasi hiyo kwa miaka mitano.

Dkt Ndugulile ni nani?

Akiwa na taaluma ya udaktari, Dkt Ndugulile amebobea katika afya ya umma. Aliwahi kuhudumu kama Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, kabla ya kuhamishiwa kwenda Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Kwa sasa, Dkt Ndugulile ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na pia ni mbunge wa jimbo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels