Uganda: Watu 11 wapoteza maisha kufuatia mlipuko wa lori la mafuta

Watu 11 wamefariki dunia baada ya lori la mafuta kupinduka na kulipuka karibu na mji mkuu wa Uganda, Kampala siku ya Jumanne.

By Edward Josaphat Qorro
Lori linasemekana lilipata hitilafu ya breki kabla ya kupinduka  / Picha: Reuters / Reuters

Lori lililokuwa limesheheni mafuta lilipoteza muelekeo, kupinduka na kisha kulipuka na kuua watu 11, kulingana na Idara ya Polisi nchini Uganda.

Tukio hilo lilitokea katika eneo la njia ya panda, lililo katika mji wa Kigogwa, kilomita 25 kutoka mji mkuu wa Uganda, Kampala.

"Idadi ya watu walipoteza maisha hadi sasa ni 10, lakini kuna taarifa za majeruhi zaidi,"alisema Charles Lwanga, Mkuu wa Wilaya wa eneo hilo katika taarifa ya awali.

Kulingana na Lwanga, lori hilo lilipata hitilafu ya breki kabla ya kutokea kwa ajali hiyo.

Wizi wa mafuta

"Watu 10 waliungua kwa moto baada ya kikundi cha watu kuamua kuiba mafuta kutoka kwenye lori hilo," alisema.

Magari ya kubebea wagonjwa yalielekea katika eneo la tukio kwa lengo la kuwawahisha majeruhi hospitali.

Hata hivyo, moto huo ulidhibitiwa, ili kuepusha kusambaa kuelekea kituo cha mafuta kilichokuwa karibu.

Watu 19, walipoteza maisha baada ya lori la mafuta kugonga magari mengine na kulipuka nchini Uganda, katika tukio lililotokea Agosti 19, 2019.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels